Na mwandishi wetu
Kocha Mkuu wa Yanga, Nasreddine Nabi amesema licha ya timu yake kupata ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Marumo Gallants ya Afrika Kusini, hajaridhishwa na kiwango kilichooneshwa na wachezaji wake katika mchezo huo.
Mchezo huo wa mkondo wa kwanza wa hatua ya nusu fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika ulichezwa jana Jumatano jioni kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam.
Nabi alisema anasikitika kwa kuwa walitengeneza nafasi nyingi kipindi cha kwanza cha mchezo huo lakini walishindwa kuzitumia ipasavyo tofauti na alivyotarajia.
“Mechi ilikuwa ngumu, kipindi cha kwanza tulitengeneza nafasi nyingi hatukupata magoli. Ninachosikitika hatukutumia nafasi kama nilivyowafundisha wachezaji wangu kwenye mazoezi, walicheza tofauti kabisa,”alisema Nabi.
Kuhusu Marumo, Nabi alisema: “Siwezi kusema ni timu dhaifu, tofauti kidogo ipo kwenye safu yao ya ulinzi ila ni wazuri wana timu nzuri, timu yangu ndio iliyokuwa na matatizo kwa sababu wachezaji wangu hawakucheza vizuri.”
Alisema katika mchezo wa marudiano utakaopigwa Mei 17, mwaka huu Afrika Kusini kila mchezaji anatakiwa kufahamu wajibu wake kwa kufanya kazi kama alivyoelekezwa kwani kazi bado haijaisha.
Kwa upande wa Kocha wa Marumo, Dylan Kerr alisema anasikitika kwa timu yake kushindwa kuzitumia nafasi nne walizotengeneza kipindi cha kwanza licha ya kumiliki mpira.
“Tulipata nafasi nne za kufunga, tulimiliki mpira lakini umaliziaji wetu haukuwa bora, tunapaswa kwenda kurekebisha makosa yetu na kujipanga kwa mchezo wa pili,” alisema.