Na mwandishi wetu
Kocha Msaidizi wa Yanga, Cedric Kaze amesema kurejea uwanjani kwa Khalid Aucho na Denis Nkane kumeongeza matumaini ya kufanya vizuri kwenye mchezo wao wa Ligi Kuu NBC dhidi ya Namungo.
Nyota hao walikosekana kwenye michezo kadhaa ya timu hiyo kutokana na kuwa majeruhi, Aucho alikuwa akisumbuliwa na kifundo cha mguu na Nkane alipata maumivu ya nyonga kwenye mchezo wa ligi dhidi ya Coastal Union, Desemba, mwaka jana.
Kaze ameeleza kuwa kupona kwa wachezaji hao kunaongeza upana wa kikosi chao na hiyo ni faida kwao kutokana na ugumu wa ligi ulivyo na mahitaji ya kutaka ushindi.
“Unapokuwa kwenye kipindi kama hiki cha kutetea ubingwa unahitaji wachezaji wako wote bora kuwa timamu, sasa Aucho na Nkane wamerudi katika kipindi muhimu ambacho timu ilikuwa inahitaji uwepo wao naamini wamekuja kuongeza kitu,” alisema Kaze.
Kocha huyo ameendelea kueleza kuwa shabaha yao kubwa msimu huu ni kuhakikisha wanatetea taji lao la ligi kuu, hivyo baada ya kurejea kwa wachezaji wao kwenye kikosi chao kwa sasa wanawakosa wachezaji wawili pekee ambao ni kipa Aboutwalib Mshery aliye majeruhi na kiungo Feisal Salum aliye nje ya kikosi kwa masuala ya kimkataba.
Yanga ambao ndio mabingwa watetezi wa ligi kuu wapo kileleni mwa msimamo wa ligi kwa pointi 56 katika michezo 21 na Jumamosi ya wiki hii wataikabili Namungo FC ikiwa ni mchezo wa raundi ya 22.