London, England
Kocha wa Tottenham Hotspur, Antonio Conte amesema ana furaha na wachezaji alionao katika timu hiyo lakini watakuwa tayari iwapo fursa sahihi ya usajili itajitokeza katika dirisha dogo la Januari.
Baada ya mapumziko ya kipindi cha fainali za Kombe la Dunia 2022 zilizofikia tamati Jumapili iliyopita, Spurs itaanza mbio za Ligi Kuu England Jumatatu dhidi ya Brentford.
“Kama kutakuwa na fursa za kukiimarisha kikosi tutafanya kitu, unajua siasa zetu zilivyo na tunajaribu kuzifuata siasa hizo na kuiboresha timu,” alisema Conte katika mkutano wake na waandishi wa habari jana Ijumaa.
“Siasa zetu zinahusu wachezaji wa umri mdogo ambao hawana mishahara mikubwa, tutasaini wachezaji ambao wanaweza kuwa hapa kuendana na dira ya klabu hii, tofauti na hivyo tutaendelea na wachezaji hawa, ninafuraha kuwa nao,” alisema Conte.
Katika hatua nyingine, Conte alisema kipa namba moja wa timu hiyo ambaye pia anaidakia timu ya Taifa ya Ufaransa iliyopoteza taji la dunia mbele ya Argentina, Hugo Lloris hatokuwa katika kikosi cha kwanza cha timu hiyo katika mechi na Brentford.
“Ni muhimu pia baada ya fainali za Kombe la Dunia kuwapa hawa wachezaji muda wa kupumzika, Crisan Romero pia (beki wa Argentina) naye atakuwapo katika mechi ijayo dhidi ya Aston Villa,” alisema Conte.
Conte aliyejiunga na Spurs Novemba mwaka jana kwa mkataba wa miezi 18 hata hivyo hakuwa tayari kuzungumza lolote kuhusu mkataba wake na klabu hiyo, alipoulizwa swali hilo alisema kwamba mechi na Brentford ni muhimu zaidi kwa sasa.
