Manchester, England
Kocha wa Man United, Erik ten Hag amesema kwamba alimuweka kando, Alejandro Garnacho (pichani) baada ya mechi mbili za awali kwa kuwa kiwango cha mchezaji huyo hakikuwa juu kiasi cha kutosha.
Garnacho alikuwa katika kikosi cha kwanza katika mechi dhidi ya Wolves na Tottenham zilizochezwa mwezi Agosti lakini aliachwa katika mechi tano kabla ya kurudi kikosi cha kwanza jana Jumanne dhidi ya Crystal Palace katika mechi ya Carabao ambayo Man United ilishinda kwa mabao 3-0.
“Utaona katika mechi za mwanzo za msimu tulikuwa tukimpanga lakini mchango wake haukuwa mkubwa kiasi cha kutosha,” alisema Ten Hag akimzungumzia mchezaji huyo ambaye ndio kwanza ana miaka 19.
“Unajua wakati wote hiyo ni hatari kwenye mechi pale anapokuwa hachezi vizuri, ni lazima ajifunze anapofanya kazi yake katika kukaba, ana nafasi yake na wakati wote atakuwa tishio kwa sababu ana sifa zote,” alisema.
“Nafikiri ni jambo la kawaida kwa mchezaji wa umri wake bado ana nafasi ya kuwa bora, kila mtu anampenda, mashabiki wanampenda, timu inampenda, na mimi nampenda lakini ni lazima tumtake awe mwenye kujitoa kwa ajili ya timu,” alisema Ten Hag.
Baada ya kumpa nafasi Garnacho, Ten Hag ameendelea kumfungia mlango, Jodan Sancho ambaye ameondolewa kikosi cha kwanza baada ya kutofautiana na kocha huyo ingawa amewapa nafasi Mason Mount, Raphaël Varane na Harry Maguire.