Na mwandishi wetu
Kampuni ya michezo ya kubashiri ya SportPesa imesikitishwa na uongozi wa klabu ya Yanga kukiuka makubaliano kama wadhamini wao wakuu baada ya klabu hiyo kutangaza na kuzindua jezi za mdhamini mwingine.
Yanga kwenye hafla waliyoifanya hivi karibuni jijini Dar es Salaam waliitangaza Kampuni ya Haier kama wadhamini wao kuelekea mechi za hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika zinazotarajia kuanza Februari 12, mwaka huu.
Hata hivyo Rais wa Yanga, Hersi Said akizungumzia udhamini huo katika hafla hiyo alisema wamelazimika kuiondoa SportPesa kifuani kwa sababu Shirikisho la Soka Afrika (Caf) haliruhusu timu kuwa na mdhamini ambaye ni mshindani wa mdhamini wa mashindano ya Caf, 1xbet.
Sportpesa Jumatano hii imetoa tamko juu ya hilo huku ikiwafahamisha wateja wake na umma kuwa bado ni mdhamini mkuu wa klabu hiyo na ina haki ya kipekee ya kuwa kifuani mwa jezi ya Yanga kwa miaka ya soka 2022 mpaka 2025.
“Ombi la Yanga kupata mfadhili mwingine kwa ajili ya hatua inayofuata ya mashindano ya Caf lilikuwa ni kukiuka makubaliano yetu na lilitukatisha tamaa sana lilipowasilishwa kwetu.
“SportPesa inafahamu kikamilifu maagizo na sheria za Caf kuhusu utangazaji/ufadhili uliopo na ilikuwa imetumia kauli mbiu ya ‘Visit Tanzania’ kuchukua nafasi yetu ili kufuata masharti yanayohitajika kutoka kwa Caf.
“Kampeni hii mbadala ya ‘Visit Tanzania’ ilifanikiwa kuitangaza nchi nzima kwa misimu miwili iliyopita ya Caf, lakini pendekezo letu lilikataliwa kwa kuwa klabu ilikuwa tayari imeamua kuuza haki hizi bila kujali masharti ya kimkataba yaliyopo na SportPesa.
“SportPesa inahifadhi haki yake ya kuomba fidia na msaada kutoka kwa mamlaka husika kwa uharibifu uliosababishwa,” ilieleza taarifa hiyo iliyowekwa na SportPesa kwenye kurasa zake za mitandao ya kijamii.
Upande wa Yanga ulitafutwa kueleza juu ya tamko hilo la SportPesa ambapo Hersi alijibu kwa kifupi: “Tutatoa taarifa rasmi kwa hiyo kuweni na subira, tutatoa taarifa, watu wasubiri taarifa rasmi kutoka Yanga.”