Na mwandishi wetu
Kocha Mkuu wa Singida Fountain Gate, Hans Pluijm ameeleza kufurahishwa na usajili wa beki mpya wa timu hiyo, Joash Onyango, akikiri ujio wake una mantiki kubwa kuelekea michuano ya msimu ujao kimataifa.
Beki huyo ilibainika ametua Singida jana kwa mkopo akitokea Simba SC alikoelezwa amebakiwa na mwaka mmoja katika mkataba wake na sasa anakwenda Singida, FG, timu ambayo msimu ujao itashiriki michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika.
Pluijm ameiambia GreenSports leo Jumamosi kuwa mchezaji huyo wa zamani wa Gor Mahia ni muhimu katika kikosi chao kuelekea msimu ujao kutokana na uzoefu, mtazamo wa mechi ngumu, uongozi na ubora alionao.
“Ni mchezaji mzuri kwa kweli, kama unavyojua msimu ujao tuna michuano mingi ikiwemo ya kimataifa, hivyo tunahitaji mchezaji kama huyu ambaye ana uzoefu mkubwa, uongozi, ubora na pia anafahamu namna ya kusoma mechi ngumu, ni faida kubwa tuliyonayo kuelekea msimu ujao,” alisema Pluijm.
Kocha huyo wa zamani wa Yanga na Azam, alieleza kuwa ndiyo kwanza wameanza kusajili wakitarajia kusuka kikosi kikubwa na kipana zaidi ya walichokuwa nacho msimu uliopita ili kufikia ndoto walizonazo.
Ukiachana na Onyango, mchezaji mwingine anayetajwa kumalizana na Singida kutoka Simba ni kipa Beno Kakolanya huku duru mbalimbali za michezo zikimtaja kiungo Jonas Mkude naye kuwa yuko njiani kumalizana na timu hiyo iliyopanda daraja kushiriki ligi kuu msimu uliopita.