London, England
Kocha wa Chelsea, Enzo Maresca amepinga madai kwamba kuna tatizo la utovu wa nidhamu katika timu yake licha ya timu hiyo kupata kadi nyekundu katika mechi na Benfica na hivyo kuwa kadi nyekundu ya tatu katika mechi nne.
Chelsea Jumanne ikiwa nyumbani ilicheza na Benfica na kupata ushindi wa bao 1-0 katika Ligi ya Mabingwa Ulaya, mechi ambayo pia ilimshuhudia kocha wa zamani wa Chelsea, Jose Mourinho kwenye dimba la Stamford Bridge akiwa na Benfica.
Katika mechi hiyo, Joao Pedro aliyeingia dakika ya 61, alitolewa katika dakika za nyongeza za mchezo huo baada ya kupewa kadi ya pili ya njano kwa kumchezea rafu mbaya Leandro Barreiro wa Benfica.
Tukio hilo la Pedro lilitanguliwa na la Robert Sanchez aliyepewa kadi nyekundu katika mechi na Man United na Trevoh Chalobah aliyekutana na adhabu kama hiyo katika mechi na Brighton kama ilivyokuwa kwa Nicolas Jackson aliyekutana na adhabu hiyo mara mbili msimu uliopita katika mechi dhidi ya Newcastle na Flamengo.
Chelsea ilipoteza mechi zote hizo na katika hali iliyoonesha dhihaka, Maresca alisema, “Walau tulijifunza namna ya kushinda mechi kupitia kadi nyekundu, lakini vyovyote ilivyo ni matukio ya dakika mbili au tatu za mchezo.”
“Wakati wote huwa napenda kuona matukio ya mchezaji mmoja mmoja, nafikiri kadi nyekundu katika mechi na Newcastle na Flamengo zilitokana na rafu mbaya lakini Sanchez naye akapewa kadi si kwa rafu mbaya, ni kwa sababu alikuwa akilinda goli,” alisema Maresca.
Akifafanua zaidi Maresca pia alisema kwamba Chalobah ni kwa sababu alitaka kulinda goli ma Joao hakumgusa mchezaji wa timu pinzani ingawa tukio zima (muelekeo wa mguu) lilikuwa la hatari na kwake (Maresca) hana sababu ya kuwa na hofu kuhusu nidhamu ya timu yake.
