London, England
Mwanzo mbaya wa Liverpool kwenye Ligi Kuu England inawezekana umezikwa Jumamosi hii baada ya timu hiyo kuichakaza Bournemouth mabao 9-0 huku Arsenal ikiendeleza wimbi la ushindi kwa kuichapa Fulham mabao 2-1 na kujiimarisha kileleni
Ushindi mnono wa Liverpool umekuja siku moja baada ya kocha wa timu hiyo, Jurgen Klopp kusema kuwa wameuanza mimu vibaya baada ya sare mbili na kipigo cha 2-1 mbele ya Man United hivyo akawataka wachezaji waongeze bidii kwa asilimia 100 au zaidi na wawe na shauku ya mafanikio.
Wachezaji hao wamemjibu kwa karamu ya mabao ambayo inatoa kila dalili kwamba timu hiyo sasa ndiyo inaanza na hivyo wapinzani wake wakae tayari.
Kwa ushindi huo mnono wa idadi ya mabao tisa, Liverpool wanakuwa wamekifanya kile kilichowahi kufanywa na Manchester United mara mbili, mwaka 1995 dhidi ya Ipswich na mwaka jana dhidi ya Southampton kama ambavyo Leicester City nao walifanya hivyo dhidi ya Southampton mwaka 2019.
Karamu ya mabao ya Livepool ilianzia dakika ya tatu kwa bao la Luiz Diaz aliyefuatiwa na Harvey Elliot dakika mbili baadaye kabla ya Alexander-Arnold kuongeza la tatu dakika ya 28 wakati bao la nne lilifungwa na Robert Firmino dakika ya 31 na Virgil van Djik kuandika bao la tano dakika ya 45 na timu hizo kwenda mapumziko.
Mikosi kwa Bournemouth ilianza tena dakika moja baada ya mapumziko, Chris Mepham alipojifunga na kuizawadia Liverpool bao la sita, Firmino tena akaandika bao la saba dakika ya 62 kabla Carvalho hajapachika la nane dakika ya 80 na Diaz akaongeza la tisa dakika ya 85, ambalo ni bao lake la pili katika mechi hiyo.
Arsenal kama kawa
Arsenal nayo iliendeleza wimbi lake la ushindi katika ligi hiyo baada ya kuilaza Fulham mabao 2-1 na hivyo kupata ushindi wa nne mfululizo huku ikiendelea kujiimarisha kileleni ikiwa na pointi 12 na ni timu pekee iliyoianza ligi hiyo hadi sasa bila sare wala kupoteza mechi yoyote.
Arsenal ndiyo iliyoanza kufungwa bao lililopachikwa wavuni dakika ya 56 na Aleksandr Mitrovic aliyeuwahi mpira ambao ulionekana kudhibitiwa na Gabriel lakini Martin Odegaaard aliisawazishia Arsenal bao dakika ya 64 na kuibua matumaini mapya kabla, Gabriel hajafuta kosa alilolifanya kwa kuipatia Arsenal bao la pili lililotokana na mpira wa kona zikiwa zimebaki dakika tano filimbi ya kumaliza mchezo kupulizwa.
Haaland aibeba City, United yapeta
Mshambuliaji mpya wa Manchester City, Erling Haaland leo ameonyesha thamani yake baada ya kupiga hat trick (mabao matatu) na kuiwezesha timu yake kutoka uwanjani na ushindi wa mabao 4-2 dhidi ya Crystal Palace baada ya kuwa nyuma kwa mabao 2-0.
Man City ambao ndio mabingwa watetezi, waliianza mechi hiyo vibaya baada ya kupachikwa bao dakika ya nne tu ya mchezo huo bao ambalo Stones alijifunga lakini ikatandikwa tena bao jingine dakika ya 21 mfungaji akiwa na Andersen na hivyo timu hizo kwenda mapumziko, City ikiwa nyuma kwa mabao 2-0.
Bernando Silva alianza kuandika bao la kwanza kwa City katika dakika ya 53 kabla Haaland hajafanya yake katika dakika za 62, 70 na 81 na kuwafanya mashabiki wa City watoke uwanjani Etihad vifua mbele wakiwa na pointi zao tatu.
Wakati City wakijivunia ushindi huo mahasimu wao wa jiji la Manchester, Man United nao si haba ushindi wa bao 1-0 walioupata dhidi ya Southampton una maana kubwa kwa kocha Erik ten Hag ambaye baada ya kuanza vibaya mechi mbili za mwanzo, timu yake iliibuka na ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya mahasimu wao Liverpool wiki iliyopita.
Ushindi huo uliotokana na bao pekee la Bruno Fernandes dakika ya 55 unatosha kupewa tafsiri ya mwendelezo wa ushindi hasa kwa wapinzani wao ambao walianza kuwatoa katika mbio za kulisaka taji hilo kwa kuamini kwamba ushindi dhidi ya Liverpool ulikuja kwa bahati.
Matokeo ya mechi nyingine za ligi hiyo ni kama ifuatavyo…
Southampton 0-1 Man Utd
Brentford 1-1 Everton
Brighton 1-0 Leeds
Chelsea 2-1 Leicester
Liverpool 9-0 Bournemouth
Man City 4-2 Crystal Palace
Arsenal 2-1 Fulham
Ligi hiyo itaendelea Jumapili hii kwa mechi zifuatazo…
Aston Villa v West Ham Saa 10:00 alasiri
Wolverhampton v Newcastle Saa 10:00 alasiri
Nottingham v Tottenham, Saa 10:00 alasiri
