Na mwandishi wetu
Ugumu wa masharti aliyopewa, Yanick Bangala na klabu ya Yanga inadaiwa ndiyo yanayomchelewesha mchezaji huyo kuachana na timu hiyo hadi sasa zikiwa zimesalia siku nne kabla ya kufungwa dirisha la usajili.
Meneja wa Bangala, Trovisa Bashisha amesema licha ya kukutana na uongozi wa Yanga juu ya barua yao waliyowasilisha ya kutaka kuondoka lakini wamepewa sharti la kiungo huyo kutosajili timu nyingine Tanzania.
“Barua ya kutaka kuondoka iliandikwa muda tu na Yanga wanayo hiyo barua na lengo ni mchezaji ametaka kuondoka akatafute changamoto nyingine. Yanga walikutana naye lakini mambo hayakwenda vizuri.
“Timu inayomuhitaji Bangala ipo lakini Yanga ndio wanakataa ndio maana pia walisema wanaweza kuachana naye lakini asicheze hapa Tanzania,” alisema meneja huyo na kuongeza:
“Bangala hajakubaliana na hilo, huwezi kumwambia mchezaji asicheze hapa Tanzania wakati kuna timu nzuri tu hapa (Tanzania), Bangala anazipenda pia.”
Taarifa zaidi zinaeleza kuwa mchezaji huyo ambaye ana mkataba wa mwaka mmoja na Yanga, anawaniwa na timu ya Azam inayotaka kuongeza nguvu kuelekea michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika itakayoshiriki msimu ujao.
Hata hivyo, ujio wa beki Gift Fred kutoka SC Villa ya Uganda nao unatajwa kuwa sehemu ya Yanga kujiandaa na maisha mapya kikosini bila Bangala aliyeibuka mchezaji bora wa Ligi Kuu Bara msimu wa 2021-22.
GreenSports ilimtafuta Makamu wa Rais wa Yanga, Arafat Haji kufahamu sakata hilo kwa upande wao lakini simu yake ya mkononi iliita bila ya kupokelewa huku simu ya Ofisa Habari wa Yanga, Ali Kamwe nayo ikiita bila ya majibu na wakati mwingine ikikatwa.
Soka Bangala adai kupewa masharti magumu
Bangala adai kupewa masharti magumu
Read also