Budapest, Hungary
Sevilla jana Jumatano imeweka rekodi ya kulibeba taji la Europa Ligi kwa mara ya saba ikiilaza AS Roma kwa penalti 4-1 huku kocha wa Roma, Jose Mourinho akiitupa medali ya shaba aliyopewa.
Ushindi wa Sevilla ambao ulitokana na sare ya bao 1-1 kabla ya mikwaju ya penalti, umekuwa tukio baya kwa Mourinho ambaye alikuwa na rekodi ya kutopoteza hata mara moja mechi ya fainali Ulaya.
Mourinho ambaye tayari ana mataji matano ya Ulaya na jana alikuwa akijiandaa kubeba taji lake la sita kabla ya Sevilla kumkwaza, kitendo chake cha kuitupa medali hiyo kilishangaza wengi.
Kocha huyo wa zamani wa klabu za Chelsea, Man United, Tottenham, Real Madrid na Inter Milan, kama kawaida yake hakukosa jibu, “hivyo ndivyo nilivyofanya, siihitaji medali ya fedha (silver) kwa hiyo niliigawa.”
“Nataka kubaki Roma lakini wachezaji wangu wanahitaji zaidi, nami nahitaji zaidi, sitaki kupambana tena katika hili, nimechoka kuwa kocha, kuwa mzungumzaji, msemaji wa klabu,” alisema.
Mourinho jana alikuwa akiwania kuipuku rekodi ya kocha mkongwe Mtaliano, Giovanni Trapattoni ambaye ana rekodi ya kushinda fainali tano za Ulaya na kama angeshinda jana angekuwa na rekodi ya ushindi wa mechi sita za fainali.
Mechi ya Roma na Sevilla pia iliandamana na rekodi nyingine ya kadi 13 za njano zilizotolewa katika mechi hiyo akiwamo Mourinho ambaye naye alipewa kadi hiyo.
Mourinho ambaye imekuwa ikidaiwa kwamba yuko mbioni kuihama Roma, alikataa kuzungumza lolote kuhusu mambo yake ya baadaye ingawa bado ana mkataba na Roma utakaofikia ukomo 2024, PSG na Real Madrid zinadaiwa kumtaka.
“Mambo yangu ya baadaye? Niko makini, nimesema miezi michache iliyopita, kwamba nikiwa na mazungumzo na klabu yoyote nitawaambia wamiliki, siwezi kufanya chochote kwa siri,” alisema Mourinho.
Katika mechi hiyo, Roma ndiyo iliyokuwa ya kwanza kupata bao lililofungwa na Paolo Dybala lakini bao la kujifunga na Gianluca Mancini lilifanya matokeo yawe sare ya bao 1-1.
Kwenye mikwaju ya penalti, baada ya Roma kukosa penalti mbili, Gonzalo Montiel ambaye pia ndiye aliyeifungia Argentina bao la ushindi kwenye fainali za Kombe la Dunia, jana pia ndiye aliyeifungia Sevila bao la ushindi lililowapa taji la saba la Ulaya.