London, England
Mshambuliaji wa Tottenham Hotspur, Harry Kane sasa ndiye mfungaji anayeongoza kwa kufunga mabao mengi katika historia ya klabu hiyo akifikisha mabao 267 na kumpiku, Jimmy Greaves mwenye mabao 266.
Kane alifunga bao lake la 267 na klabu hiyo jana Jumapili katika ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Man City katika mechi ya Ligi Kuu England au EPL na sasa anataka kumpiku Alan Shearer mwenye rekodi ya mabao 260 kwenye EPL.
Akizungumzia azma yake ya kumpiku Shearer baada ya kuwa tayari amempiku Greaves, Kane alisema, “Alan ameweka rekodi inayotakiwa kuvunjwa, tutaona kama nitaivunja.”
Katika EPL, Kane amefikisha jumla ya mabao 200 hadi sasa na hivyo ana kazi ya kuzifumania nyavu mara 60 ili kuifikia rekodi ya Shearer na baada ya hapo kujipanga kuivunja na kuweka rekodi mpya.
“Nina hakika Shearer atakuwa akiangalia lakini sina hakika kama atakuwa mwenye furaha au la, bado nina mabao mengi ya kufunga, najisikia vizuri,” alisema Kane.
Kwa kipindi kirefu, Greaves aliyeanzia kutamba Chelsea amekuwa akijivunia rekodi ya mabao 266 aliyoyafunga akiwa na Spurs katika mechi 379 kati ya mwaka 1961 hadi 1970 kabla ya Kane kuifikia rekodi hiyo mwezi uliopita kwa kufikisha mabao 266 na kuivunja rasmi Jumapili alipofikisha mabao 267.
Kane mwenye umri wa miaka 29 yeye alianza kuichezea Spurs mwaka 2011 na hadi sasa amecheza jumla ya mechi 416 akiwa na timu hiyo.
Katika timu ya Taifa, Kane pia anawania rekodi ya kuwa mfungaji mwenye mabao mengi kwani kwa sasa amefungana na mshambuliaji wa zamani wa timu hiyo, Wayne Rooney kila mmoja akiwa na mabao 53 na hivyo anahitaji bao moja ili kumpiku Rooney.