Na mwandishi wetu
Makamu Rais wa Klabu ya Yanga, Arafat Haji ameeleza kutofurahishwa na mwenendo mbaya wa timu yao ya wanawake, Yanga Princess na kuahidi kurekebisha baadhi ya mambo ili wapate furaha upande huo pia.
Haji alisema hayo leo Jumanne kupitia ukurasa wake wa mtandao wa Instagram ambapo alieleza kuwa bado wanaendelea kufanya maboresho ya kiufundi kwenye maeneo kadhaa, kuanzia ndani ya uwanja hadi nje ya uwanja.
“Tutakubaliana kwa pamoja kwamba ilipo leo Yanga Princess sio ilipokuwa misimu kadhaa nyuma! Taratibu mabadiliko yanaendelea kufanyika na muda si mrefu watu wataanza kufurahia matunda,” aliandika Haji.
Alieleza, nguvu kubwa ya maboresho ilianza kwenye timu yao kubwa ya wanaume na baada ya kukaa vizuri na kubeba mataji kadhaa, sasa wameanza taratibu kuiboresha Yanga Princess na kushuka hadi timu zao za vijana za umri chini ya miaka 17 na 20.
Alisema mabadiliko yanapofanyika matokeo hayaonekani kwa haraka badala yake ni mchakato unaohitaji muda kwani hata walipoanza kwa timu ya wanaume iliwachukua misimu miwili kabla ya kuanza kubeba mataji.
Yanga Princess inashika nafasi ya nne kwenye msimamo wa Ligi Kuu ya Wanawake (TWPL) ikiwa na pointi 12 baada ya kucheza mechi sita ikishinda mechi nne na kufungwa michezo miwili.
Soka Bosi haifurahii Yanga Princess
Bosi haifurahii Yanga Princess
Read also