Na mwandishi wetu
Timu ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars imeanza na mguu mbaya mashindano ya Fifa Series nchini Azerbaijan baada ya kuchapwa bao 1-0 na Bulgaria katika mechi iliyopigwa leo Ijumaa.
Bulgaria walipata bao hilo pekee dakika sita baada ya mapumziko mfungaji akiwa nahodha wa timu hiyo, Kiril Despedov ambaye alifunga kwa mpira wa adhabu ndogo.
Stars licha ya kupoteza mchezo huo lakini iliweza kuonesha uhai mfano katika dakika ya 28, Kibu Denis aliwazidi kasi mabeki wa Bulgaria na kufumua shuti lililogonga mwamba kabla ya kumkuta Feisal Salum ‘Fei Toto’ ambaye akiwa sehemu nzuri ya kufunga alipiga shuti lililopaa.
Fei Toto kwa mara nyingine dakika ya 73 alishindwa kuyatumia makosa ya safu ya ulinzi ya Bulgaria baada ya kuunasa mpira akiwa karibu na mlinda mlango lakini shuti alilopiga lilipaa kwa mara nyingine.
Katika mchezo huo Stars iliongeza kasi ya mashambulizi hasa kipindi cha pili baada ya kocha Hemed Suleiman ‘Morocco’ kufanya mabadiliko kwa kuwatoa, Kibu, Tarryin Allakakhia, Maino Danilo na Haji Mnoga.
Nafasi za wachezaji hao waliingia Clement Mzize, Lusajo Mwaikenda, Abdul Seleman Sopu na Charles Mmombwa, mabadiliko ambayo licha ya kuongeza kasi ya mashambulizi lakini hayakuzaa bao.
Katika mechi hiyo, Stars ilipata pigo mapema dakika ya 31 baada ya kipa Aishi Manula kuumia na kulazimika kutolewa na nafasi yake kuingia Kwesi Kawawa.
Baada ya matokeo hayo, Stars sasa inasubiri kucheza mechi yake ya pili ya michuano hiyo dhidi ya Mongolia, mechi ambayo itapigwa Jumatatu ijayo.
Kimataifa Stars yaanza na mguu mbaya Azerbaijan
Stars yaanza na mguu mbaya Azerbaijan
Read also