Na mwandishi wetu
Klabu ya Yanga imeibuka na kuzima taarifa zinazohusishwa na kuuzwa kwa mshambuliaji wao, Fiston Mayele anayedaiwa kuwa amemalizana na timu ya Kaizer Chiefs ya Afrika Kusini.
Mapema leo kuliibuka tetesi hizo kutoka kwa mwandishi wa Ghana anayefahamika kwa jina la Nuhu Adams akieleza juu ya kukamilika kwa dili hilo la miaka mitatu na kwamba muda wowote atatangazwa kwenye kikosi cha Kaizer.
Hata hivyo, Kaimu Mtendaji Mkuu wa Yanga, Senzo Mazingiza ameeleza kuwa taarifa hizo hazina ukweli wowote na haelewi inakuwaje zinatangazwa hivyo huku akiwahakikishia mashabiki wa timu hiyo kuwa msimu ujao wataendelea kupata huduma ya mshambuliaji huyo raia wa Jamhuri ya Demokrasi ya Congo.
Senzo alisisitiza kuwa hawajapata barua wala makubaliano yoyote ya kumuuza mchezji huyo, akiongeza kuwa kipindi hiki watu watasikia mengi kwa kuwa ndiyo wakati wa wachezaji kuhama na taarifa nyingi kama hizo hata kama hazina ukweli.
“Sijui niseme hii ni uvumi, lakini hakuna barua rasmi ya klabu wala chochote, haya mambo yatakuwa ya mitandaoni si kweli. Mayele ni mchezaji wa Yanga haendi kokote atakuwa na Yanga msimu ujao, ataendelea kuwepo hapa.
“Kumbuka huu ndiyo ule msimu wa uvumi wa kuuzwa na kuhama kwa wachezaji kwa hiyo ni uvumi, hatuwezi kusema tupo naye wakati hatupo naye, kwa sasa Mayele ni mchezaji wetu na yupo mapumzikoni kwa ajili ya msimu mpya,” alisema Senzo raia wa Afrika Kusini.
Kuhusu kiungo wa Burkina Faso, Stephane Aziz Ki anayekipiga Asec Mimosas, Senzo alibainisha kuwa wameshamalizana naye muda mrefu na kwamba muda wowote watamtambulisha, akiwataka mashabiki wawe na subira siku si nyingi ataweka wazi usajili wote wa msimu ujao.
Mayele ambaye amekuwa gumzo nchini kutokana na uwezo wake wa kufunga mabao anaouonesha tangu atue Yanga msimu huu akitokea AS Vita. Amefunga mabao 16 akizidiwa bao moja na kinara, George Mpole wa Geita Gold aliyefunga mara 17.
Soka Mayele haendi Kaizer Chiefs-Senzo
Mayele haendi Kaizer Chiefs-Senzo
Green SportsAuthor / Greensports Media LTD
Greensports author
Read also
