Madrid, Hispania
Winga wa Villarreal ya Hispania, Alex Baena (pichani) amelalamikia kupokea taarifa za kutishiwa kifo yeye na familia yake baada ya kudaiwa kumtakia mabaya kiungo wa Real Madrid, Federico Valverde.
Baena tayari amewasilisha malalamiko polisi akilalamika kutishwa baada ya timu yake kutoka na ushindi wa mabao 3-2 dhidi ya Real Madrid katika mechi ya La Liga iliyochezwa Jumamosi iliyopita.
Klabu ya Villarreal katika taarifa yake ilidai kwamba mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 21 alibughudhiwa wakati akielekea kwenye basi la timu hiyo muda mfupi baada ya mechi.
“Jumamosi iliyopita nilibughudhiwa tena na mwenzangu katika soka baada ya mechi dhidi ya Real Madrid,” alisema Baena ingawa hakumtaja Valverde.
“Baada ya kutokea hilo ujumbe ukaanza kunijia, huenda umeandaliwa na watu wa kundi lake, ujumbe ambao ulisema kwamba eti nimeitakia mabaya familia yake,” alisema Baena.
Mpenzi wa Valverde, Februari mwaka huu alidai kwamba walidhani mtoto wao alifariki wakati wa ujauzito lakini baadaye ilibainika kwamba mtoto huyo alikuwa mwenye afya tele. Inadaiwa baadhi ya ujumbe ulidai kwamba Baena alilitaja tukio hilo wakati wa mechi.
Baena alisema kwamba tuhuma hizo ni uwongo mtupu lakini alisisitiza kwamba familia yake ilikutana na kauli za kashfa pamoja na kutishiwa maisha.
“Wanatumia tatizo kuhalalisha mashambulizi yao, na ukweli ni kwamba kuna uwongo unaouma kuliko kupigwa ngumi,” aliongeza Baena.
“Ubaya ambao familia yangu imefanyiwa haulingani na chochote na hauna uhalali wowote, kuna vitisho, matusi na baadhi ya ujumbe binafsi wa kuitishia familia yangu kifo,” alisema na kutaka haki itendeke.