Na Hassan Kingu
Msimu wa Ligi Kuu NBC 2022-23 umefikia ukingoni zikiwa zimesalia mechi mbili kwa kila timu kabla ya kufungwa rasmi pazia la ligi msimu huu.
Miongoni mwa timu zilizofanikiwa kutimiza ndoto zake katika ligi hiyo ni Yanga ambao wameutetea ubingwa wao baada ya mechi 28 walipoifunga Dodoma Jiji mabao 4-2 na kufikisha pointi 74 ambazo hazitafikiwa na timu nyingine.
Singida Big Stars wanachuana na Azam kwenye vita ya kumaliza nafasi ya tatu kama ilivyo vita ya Namungo na Geita Gold ya kuwania kumaliza nafasi ya tano.
Ruvu Shooting tayari imeshuka daraja lakini kuna utata kuanzia nafasi ya nane hadi ya 15, wote wanapambana kutoungana na Ruvu au kutocheza mechi za mtoano kuwania kusalia kwenye ligi hiyo msimu ujao.
Hata hivyo, utamu na ugumu wa ligi hiyo umechangiwa na uzuri, ubora, viwango na ushindani unaooneshwa na wachezaji wa timu hizo 16 zinazoshiriki michuano hiyo maarufu kwa sasa Afrika.
Kama ilivyo ada, mwisho wa msimu hugawiwa tuzo za wachezaji binafsi waliofanya vizuri kwenye nyanja mbalimbali kwa kutambua mchango wao au namba za ubora wao ndani ya msimu mzima.
GreenSports imekuandalia orodha ya baadhi ya wachezaji waliofanya vizuri zaidi na kuunda kikosi bora cha msimu huu kulingana na ubora, ubunifu na uwezo waliounesha katika timu zao na kuzisaidia kufika hapo zilipo:
-1. Djigui Diarra (Yanga)
Ubora aliounesha akiwa na Yanga tangu msimu uliopita na kutunukiwa tuzo ya kipa bora wa msimu ndicho alichoendeleza kukifanya msimu huu pia kwa kuiweka Yanga katika mikono salama ya ulinzi.
Diarra ndiye anaongoza kwa ‘clean sheet’ akiwa nazo 16 mpaka sasa akifuatiwa na Aishi Manula wa Simba aliyefanya hivyo mara 12.
Kuonesha anazidi kuimarika kila msimu, Diarra tayari amevunja rekodi ya clean sheet 15 alizoweka msimu uliopita.
Kipa huyo raia wa Mali pia ni mahiri kwenye kupanga ukuta wake wa ulinzi, ukali wa kuwashtua mabeki wake wawe makini, ujuzi wa kuanzisha mashambulizi ni miongoni mwa silaha zake zinazompa ubora wa hali ya juu.
-2. Shomari Kapombe (Simba)
Kapombe maarufu kwa mashabiki wa Simba kama Baba Esther ameendelea kuimarika kila msimu na kuthibitisha kwa mara nyingine ukongwe alionao katika ligi hiyo kutokana na kazi safi ya beki wa kulia anayoifanya.
Mbali na shughuli za ulinzi anazozifanya kwa bidii kubwa lakini pia anahusika kutengeneza nafasi nyingi za mabao za timu hiyo akiwa na pasi sita za mwisho za mabao mpaka sasa.
-3. Mohamed Hussein (Simba)
Nahodha msaidizi wa Simba, ndiye beki pekee aliyefungana kileleni kwa pasi za mabao na Kapombe. Haishangazi kufanya hivyo kutokana na ubora alionao anapopanda kwenda kushambulia.
Kasi, ujanja, namna ya kuuchezea mpira mguuni ni moja ya silaha zake adimu anapokuwa kwenye majukumu yake ya kulilinda lango la Simba na pia kufanya mashambulizi kwa ufasaha ikiwa ni jukumu lake la pili la beki wa pembeni kulingana na mifumo ya sasa.

-4. Dickson Job (Yanga)
Umbo dogo alinalo beki huyu wa zamani wa Mtibwa Sugar, halimzuii kufanya majukumu ya kikatili kwa washambuliaji wenye uchu wa mabao na wenye miili mikubwa.
Akili kubwa aliyonayo na utulivu kwenye eneo la ulinzi vimemuongezea nafasi kubwa ya kuingia katika kikosi hiki huku akiwa na uwezo wa kuanzisha mashambulizi. Job ni kati ya silaha zilizofanya Yanga ifungwe mabao machache mpaka sasa, 15.

-5. Henock Inonga (Simba)
Utulivu wa hali ya juu, umakini anapokaba washambuliaji, ubora wa kucheza mipira ya vichwa, burudani ya chenga pamoja na pasi za uhakika, ndivyo vinavyompa ubora na kuimbwa na mashabiki wa Simba kila kukicha.
Hana umbo la upambanaji lakini ‘jihad’ na akili za mpira alizonazo dhidi ya wapinzani zimekuwa nguzo kubwa kwa Simba msimu huu na kufanya Wekundu hao kuungana na Yanga kuwa timu mbili pekee zilizofungwa mabao machache mpaka sasa.
-6. Khalid Aucho (Yanga)
Kiungo wa kati mwenye uwezo wa kukaba na kuchezesha timu kutoka Uganda ni chachu nyingine ya mafanikio ya Yanga msimu huu kwenye eneo hilo muhimu la kuunganisha mawasiliano ya timu.
Aucho au ‘The Tank’ amekuwa akilitumia vyema umbo lake kubwa alilonalo kuonesha ubabe kwa wapinzani, kupokonya mipira lakini pia silaha yake ya kutokaa na mpira muda mrefu, akipiga pasi za haraka vimekuwa vikimlinda mno na kumuweka kwenye ubora kila wakati.
-7. Saido Ntibazonkiza (Simba)
Kiungo mshambuliaji huyu aliyeanza kuonesha makali yake msimu huu akiwa na Geita Gold ameendelea kuonesha kazi yake hata baada ya kuhamia Simba kwenye dirisha dogo msimu huu.
Licha ya kasi na mashuti ya uhakika aliyonayo lakini Ntibazonkiza ndiye mchezaji pekee aliyechangia mabao mengi. Amefunga mabao 10 na ametoa pasi za mwisho 12 na kumfanya kuhusika kwenye jumla ya mabao 22.
-8. Mzamiru Yassin (Simba)
Unaweza kumwita ‘kiungo punda’ kwa shughuli nzito ya kukimbizana na mipira, kuipokonya, kuitawanya na wakati mwingine kupiga pasi za mwisho kwa washambuliaji.
Sio mzuri sana wa maamuzi ya pasi za mbali lakini ni mzuri mno wa kupiga pasi fupi na kusumbua maadui eneo la tatu ya mwisho ya lango la wapinzani.
Mzamiru pia anatajwa kama miongoni mwa viungo wenye kufanya kazi kwa hesabu kubwa kulingana na maelekezo ya kocha anayoyataka akitumika kama kiunganishi cha timu inapohitaji mkakati maalum kwa wapinzani.

-9. Fiston Mayele (Yanga)
Kinara wa mabao 16 katika orodha ya wafungaji wa Ligi Kuu mpaka sasa. Anafunga kila aina ya mabao, anaimbwa kila kona kwa jihad ya kutaka kuzifumania nyavu katika kila mechi.
Ana kasi, mjanja wa kuhadaa mabeki, anapiga mashuti bila ya kusahau sifa yake ya ‘uchoyo’ ambayo imekuwa ni sababu nyuma ya mafanikio yake ya kufunga mabao mengi na kuwa tishio kwa msimu wa pili mfululizo kwenye ligi.
Mayele ni mchezaji wa pili kuhusika katika mabao mengi msimu huu baada ya Ntibazonkiza. Amehusika kwenye upatikanaji wa mabao 19.

-10. Bruno Gomez (Singida BS)
Kiungo Mbrazil mwenye ubunifu, ujanja, chenga na uwezo wa kufunga mabao ya mbali. Amethibitisha ubora wake akiwa na msimu wa kwanza Singida na kuwa moja ya chachu ya timu hiyo kufanya vizuri.
Mabao tisa aliyofunga na uwezo mkubwa anauonesha umemfanya atamkwe kwenye ofisi nyingi za viongozi wa timu kubwa za soka nchini, wengi wakivutiwa na huduma yake adhimu aliyoionesha mpaka sasa akiwa na uwezo wa kucheza nafasi zote za katikati ya uwanja.
-11. Clatous Chama (Simba)
Mbabe wa pasi za mwisho, akiwa anaongoza orodha hiyo kwa pasi 14 mpaka sasa. Ubora wake wa kuuchezea mpira, kuituliza timu vinamuweka kwenye viwango vya juu mno msimu huu.
Usisahau pia uwezo wake mkubwa wa kufunga mabao ya utulivu na ya kushangaza, faulo na kadhalika vimemfanya kuwa miongoni mwa wachezaji wa juu. Kwa kifupi Chama ni miongoni mwa viungo washambuliaji wachache wa ligi hii wanaoonesha utofauti mkubwa na wengine.

Benchi la Ufundi
Nasreddine Nabi, Cedric Kaze na Juma Mgunda
Wachezaji wa akiba
Aishi Manula (Simba), Nicholaus Gyan (Singida BS), Joyce Lomalisa, Bakari Mwamnyeto, Stephane Aziz Ki (Yanga), Yusuf Kagoma (Singida BS), James Akaminko, Ayoub Lyanga (Azam), Jean Baleke (Simba) na Eric Kaijage (Kagera Sugar).
