Turin, Italia
Turin, Italia
Kiungo Paul Pogba ameijia juu klabu yake ya zamani ya Man United akidai imemfedhehesha na sasa anataka kuithibitishia klabu hiyo kwamba ilifanya kosa kwa kushindwa kumuongezea mkataba.
Pogba aliondoka Man United hivi karibuni akiwa mchezaji huru baada ya klabu hiyo kutokuwa tayari kumuongezea mkataba na tayari amerudi katika klabu yake ya zamani ya Juventus ya Italia kwa mkataba wa miaka minne.
Kiungo huyo Mfaransa ambaye kuna wakati alisema anahitaji kujiona mwenye kupendwa ndani ya Man United, ameitupia lawama klabu hiyo katika makala maalum aliyoipa jina la Pogmentary inayotarajia kutoka Ijumaa. “Ninachofikiria ni kuwaonyesha kwamba wamefanya kosa kuchelewa kunipa mkataba na kuzionyesha klabu nyingine kwamba Manchester walifanya kosa kutonipa mkataba.” alisema Pogba.
Wakala wa zamani wa Pogba, Mino Raiola ambaye alifariki dunia Aprili mwaka huu kutokana na maradhi ambayo hayakuwekwa wazi anaonekana katika makala hiyo akimwambia Pogba kwamba Man United hawana walichompa katika mpango mzima wa kumuongezea mkataba.
Katika hilo, Pogba anajibu, “Unawezaje kumwambia mchezaji ambaye unamtaka kwamba huna cha kumpa, sijawahi kuona hilo.”
Maisha ya kiungo huyo yalianza kuwa magumu Man United na katika mechi mbili za timu hiyo dhidi ya Norwich na Liverpool alijikuta akizomewa na mashabiki wake ambao ni dhahiri walionekana kumchoka kwa kinachoonekana kutokuwa na mchango walioutarajia wakati akisajiliwa.
Mafanikio pekee anayojivunia Pogba tangu ajiunge na timu hiyo mwaka 2016 akitokea Juventus ni Kombe la Ligi na lile la Europa yaliyopatikana mwaka 2017 wakati timu hiyo ikinolewa na Jose Mourinho, kocha ambaye kwa sasa anainoa Roma ya Italia.
