Liverpool, England
Mshambuliaji wa Liverpool, Mohamed Salah amesema bado hajaamua lolote kuhusu mambo yake ya baadaye na klabu hiyo wakati huu akiendelea kudhihirisha ubora wake.
Salah hivi karibuni ameifungia Liverpool bao moja katika ushindi wa mabao 5-0 dhidi ya West Ham na kutoa pasi zilizozaa mabao mengine mawili katika ushindi huo.
Wachezaji wengine wa Liverpool, Virgil van Dijk na Trent Alexander-Arnold kama ilivyo kwa Salah nao wapo katika miezi yao sita ya mwisho kabla ya mikataba yao kufikia ukomo ingawa Salah ndiye amekuwa mjadala zaidi.
Na ingawa kumekuwa na hofu kwamba anaweza akaondoka Liverpool, Salah amesema fikra zake kwa sasa zipo katika kuhakikisha anashinda taji akiwa na timu hiyo na yuko mbali na mpango wowote wa kusaini mkataba mpya.
“Hapana hilo jambo kwa sasa lipo mbali, na sitaki kuwe na chochote kwenye vyombo vya habari, kitu pekee kilicho katika fikra zangu ni kutaka Liverpool ibebe taji la ligi, nataka kuwa mmoja wa wahusika wa jambo hilo” alisema Salah.
Alifafanua kwamba atafanya kila kilicho bora kwa ajili ya timu kushinda taji na kwa sasa ni timu chache zinazowakaribia hivyo wanahitaji kuwa makini na kuendelea na kasi yao.
Kwa upande wake kocha wa Liverpool, Arne Slot amesema hana wasiwasi na wachezaji hao waandamizi kwamba wanaweza kuanza mazungumzo na klabu nyingine Januari Mosi kwa kuwa anaamini amekuwa mwenye usimamizi wa hatma yao.
