Riyadh, Saudi Arabia
Aliyekuwa kocha wa timu ya Taifa ya Italia, Roberto Mancini ameteuliwa kuwa kocha mkuu mpya wa timu ya taifa ya Saudi Arabia ikiwa ni takriban wiki mbili baada ya kujiuzulu kuinoa timu ya Italia.
Mancini ameiongoza vyema Italia katika fainali za Kombe la Ulaya 2020 ‘Euro 2020’ na kuiwezesha kubeba taji hilo kwa kuwabwaga wenyeji England kwa penalti katika mechi iliyopigwa kwenye dimba la Wembley.
Kocha huyo mwenye umri wa miaka 58 ambaye pia amewahi kuinoa Man City, akiwa na timu ya Italia amejiwekea rekodi ya kuiongoza katika mechi 37 bila kupoteza hata moja hadi kufuzu fainali za Kombe la Dunia 2022 zilizofanyika Qatar, Novemba hadi Desemba mwaka jana.
Mancini amesaini mkataba wa kuinoa timu ya Saudi Arabia hadi mwaka 2027 na mtihani wake wa kwanza utakuwa Septemba 8 katika mechi ya kirafiki na Costa Rica itakayopigwa St James’ Park, Newcastle.
“Naamini hii ni fursa kubwa kwangu, kupata uzoefu wa soka katika nchi mpya hususan kutokana na kukuwa kwa umaarufu wa soka katika bara la Asia,” alisema Mancini.
Mancini ambaye ndiye aliyeipa Man City taji la kwanza la Ligi Kuu England, pia amewahi kuzinoa timu za Inter Milan, Lazio, Fiorentina, Galatasaray na Zenit St Petersburg.
Katika fainali za Kombe la Dunia mwaka jana, timu ya Saudi Arabia ikiwa chini ya kocha Mfaransa, Herve Renard iliushtua ulimwengu kwa kuilaza mabao 2-1 Argentina ambayo baadaye ndiyo iliyobeba taji hilo ingawa pamoja na ushindi huo, timu hiyo haikuweza kuvuka hatua ya makundi.