Na mwandishi wetu
Kocha msaidizi wa Yanga, Cedric Kaze ameeleza kuwa wapo kwenye maandalizi makali kuendeleza rekodi ya kutopoteza mchezo katika mechi yao ya kesho dhidi ya Ruvu Shooting kabla ya kuivaa Al Hilal ya Sudan.
Kaze alifafanua kwamba ushindi wa mechi na Ruvu una umuhimu kwao si tu kwa ajili ya kuendeleza rekodi ya kutopoteza mchezo lakini pia kuendeleza vizuri mbio za kutetea ubingwa wao wa Ligi Kuu ya NBC.
Pamoja na hayo, Kaze alieleza kuwa wanatarajia mchezo mgumu katika mechi hiyo itakayopigwa keshokutwa kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam kutokana na ubora wa wapinzani wao akikumbushia namna walivyowasumbua msimu uliopita.
“Wakati huu wa maandalizi ya mechi za michuano ya Afrika, pia ni muhimu kutafuta pointi tatu kuendeleza rekodi na kuweka mazingira mazuri kuelekea mechi za ligi. Mechi ya Ruvu tutaingia kwa tahadhari kubwa maana hata msimu uliopita walitupa changamoto kwenye mechi zote mbili.
“Haitakuwa rahisi ndiyo maana tunatia nguvu sana kuhakikisha tunakwenda kwenye mechi tukiwa vizuri, watu wanafikiria sana Al Hilal kama vile hakuna mechi ya ligi hapa kati na huo ndiyo mtego ambao unaweza kujikuta unapoteza kwenye ligi, kitu ambacho hatutaki kitokee,” alisema Kaze.
Yanga licha ya kuhitaji kutetea ubingwa huo lakini pia hawako tayari kuvunjiwa rekodi ya kutopoteza mchezo kwenye ligi, rekodi ambayo wameiweka tangu msimu uliopita.
“Kwenye hii mechi tunaingia tukiwa makini zaidi tukihitaji matokeo kwa kuwaheshimu tunaocheza nao tuweke nguvu zote na baada ya hapo tuendelee na mipango na mikakati ya mechi ya Al Hilal,” alihitimisha Kaze.
Katika mechi mbili za mwisho baina ya timu hizo, Yanga iliibuka na ushindi wa mabao 3-1 kwenye mechi ya kwanza kabla ya kumaliza kwa suluhu kwenye mechi ya pili walipokuwa ugenini.
Yanga ikimalizana na Ruvu, itavaana na Hilal kwenye mchezo wa raundi ya pili ya Ligi ya Mabingwa Afrika Oktoba 8 kabla ya kurudiana Oktoba 16, mwaka huu.
Soka Kaze: Tunataka rekodi kwa Ruvu Shooting
Kaze: Tunataka rekodi kwa Ruvu Shooting
Green SportsAuthor / Greensports Media LTD
Greensports author
Read also
