Riyadh, Saudi Arabia
Cristiano Ronaldo amerejea kwa mara nyingine katika kikosi cha kwanza cha Al Nassr katika mechi dhidi ya Al Fateh baada ya kuwa kwenye mgomo baridi uliomfanya akose mechi mbili zilizopita za timu hiyo.
Katika mechi hiyo iliyochezwa Jumamosi Februari 14, 2026, Ronaldo alikuwamo katika kikosi cha kwanza akiwa ndiye nahodha wa timu yake iliyotoka na ushindi wa mabao 2-0.
Akiwa sambamba na mastaa wengine wa timu hiyo kina João Félix, Sadio Mané na Kingsley Coman, Ronaldo ndiye aliyefunga bao la kwanza la timu yake katika dakika ya 18.
Al Nassr iliongeza bao la pili katika dakika ya 70 mfungaji akiwa ni Ayman Yahya, ushindi ambao umeifanya Al Nassr ijiimarishe katika nafasi ya pili ikiwa imezidiwa na vinara Al Hilal kwa tofauti ya pointi moja.
Katika wiki tatu za hivi karibuni Ronaldo alikuwa katika mgomo uliomfanya azikose mechi za Al Nassr dhidi ya Al Riyadh na Al Ittihad na kukawa na habari kwamba timu hiyo ilikuwa tayari kumruhusu aondoke.
Katika mgomo huo, Ronaldo alikuwa akilalamikia uendeshaji wa Ligi Kuu Saudi Arabia au Saudi Pro League na zaidi kitendo cha uongozi wa klabu ya Al Nassr kutoongeza nguvu katika uwekezaji wa timu kama ilivyo kwa mahasimu wao, Al Hilal.
Ronaldo hajafurahishwa na hali hiyo hasa baada ya Al Hilal kumsajili Karim Benzema kutoka Al Ittihad, Benzema nyota wa zamani wa timu ya taifa ya Ufaransa, aliwahi kucheza na Ronaldo katika klabu ya Real Madrid.
Baada ya mgomo huo, mamlaka ya uendeshaji wa ligi hiyo ilitoa taarifa yenye kutoa msisitizo kwa klabu zote kusimamia masuala yao ya kifedha na uendeshaji wa klabu kwa namna zinavyoona kuwa sahihi.
Ronaldo hadi sasa amefikisha mabao 18 katika ligi hiyo kwa msimu huu akiwa amefungana na Julian Quinones wa Al Gadsiah ambao wote wanawania kiatu cha dhahabu sawa na Ivan Toney wa Al Hilal mwenye mabao 16.
Kimataifa Ronaldo asitisha mgomo baridi
Ronaldo asitisha mgomo baridi
Read also
