Manchester, England
Kocha wa Man City, Pep Guardiola amesema hana shaka Hispania itachukua hatua sahihi kukabiliana na ubaguzi wa rangi kwenye soka.
Pep ametoa kauli hiyo baada ya mshambuliaji wa Real Madrid, Vinicius Junior kukumbana na kadhia hiyo mara kwa mara hali ambayo imeibua taharuki kwa watu mbalimbali duniani kote.
Vinicius amekumbana na kadhia hiyo kwa mara nyingine katika mechi na Valencia kwenye Uwanja wa Mestalla na tayari watu watatu wamekamatwa kwa kumtolea maneno na ishara za kibaguzi mchezaji huyo.
Kutokana na tukio hilo, Uwanja wa Mestalla umepewa adhabu ya kuzuia sehemu ya mashabiki kuingia uwanjani huku mamlaka za kisheria nchini Hispania zikiendelea na taratibu nyingine za kisheria dhidi ya wahusika.
Pep ambaye pia anatokea Hispania na amewahi kucheza soka katika La Liga na kuwa kocha kwenye ligi hiyo hata hivyo alisema hatarajii mambo kubadilika kwa haraka.
“Ni kweli kwamba ubaguzi wa rangi ni tatizo kila mahali, si kwa eneo fulani pekee, ni kila mahali kunakuwa na watu wanaofikiri kwamba wao ni bora kuliko jirani zao, sisi ni bora kuliko wengine,” alisema Pep.
“Tatizo ni kwamba kuna ubaguzi kila mahali, si tu wa jinsia bali pia katika rangi, hulka, tunaamini kwamba lugha yetu ni bora kuliko ya wengine, nchi yetu ni bora kuliko nyingine, ni mambo kama hayo,” alisema.
“Tunatakiwa kukubali muingiliano kama jambo zuri kwa wanaadamu,” alisema Pep kocha aliyejipatia mafanikio akiwa na klabu ya Barcelona.