London, England
Kocha wa Tottenham, Antonio Conte amewatupia lawama wachezaji wake akidai ni wabinafsi na kumshutumu mmiliki wa klabu kwa kuimiliki kwa muda mrefu bila kushinda lolote.
Conte ameshusha tuhuma hizo baada ya sare ya mabao 3-3 jana Jumamosi dhidi ya Southampton akidai klabu hiyo inaweza kumtimua kocha lakini mambo hayatobadilika huku akidai wachezaji hawataki kusaidiana
“Hadithi ya Tottenham ni hii ya miaka 20 ambapo kuna huyu mmiliki na hawajawahi kushinda chochote. Kwa nini?” Alihoji Conte.
Tottenham au Spurs ilikuwa ikiongoza kwa mabao mawili lakini katika dakika 15 ilijikuta ikifungwa mara mbili jambo ambalo ni kama liliamsha hasira za Conte katika mechi hiyo.
“Je tatizo ni kwa klabu tu au kwa kila kocha anayekuwa hapa? Nimewaona makocha ambao Tottenham inakuwa nao kwenye benchi, unajiweka katika hali hatarishi ya kumvuruga kocha na kulinda mazingira mengine kila wakati,” alisema Conte.
“Hadi wakati huu nimekuwa nikijaribu kuficha mambo lakini si kwa sasa tena kwa sababu hiyo narudia, hii hali niliyoiona leo (jana Jumamosi) sitaki kuiona tena kwa sababu hii haikubaliki na haikubaliki pia kwa mashabiki,” alisema Conte.
Tangu mwaka 2001 klabu hiyo ilipoanza kumilikiwa na Daniel Levy ambaye ndiye mwenyekiti, Tottenham imeshinda taji moja tu (Kombe la Ligi) ambalo walilibeba mwaka 2008.
Timu hiyo imekuwa na makocha tofauti 11 tangu wakati huo wakiwamo watatu waliokuwa katika kipindi cha mwaka 2019 alipoondoka Mauricio Pochettino ambaye aliifikisha timu hiyo katika fainali ya Ligi ya Mabingwa kabla ya kutimuliwa miezi sita baadaye.
Tottenham imetolewa katika mashindano karibu yote, kuanzia FA ilipotolewa na Sheffield United kabla ya kutolewa na AC Milan kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya na sasa Conte anasema umefika wakati wa klabu na wachezaji kila mmoja abebe jukumu lake.
“Si tu kwa klabu, kocha na maofisa, wachezaji nao ni lazima wahusike katika hali hii kwa sababu ni wakati sasa wa kubadili hii hali kama Tottenham inataka mabadiliko,” alisema Conte.
“Kama wanataka kuendelea na hali hii wanaweza kumbadili kocha, watabadili makocha wengi lakini hii hali haiwezi kubadilika, niamini mimi,” alisema.
Alipoulizwa ni kwa nini hali hiyo ipo Tottenham, Conte alisema: “Ni kwa sababu hapa wamezowea hivyo, hawachezi kwa ajili ya kitu muhimu, hawataki kucheza kama wapo katika presha ya kutaka kitu, hawataki kucheza wakiwa katika hali ya kuhimizwa na kutakiwa wapambane kupata ushindi,” alisema.
“Tuna mechi 10 na kuna watu wanafikiri tunaweza kupambana, kupambania nini katika hulka za aina hii, misimamo hii, kujituma kwa aina hii, ni kwa ajili ya nini? Nafasi ya saba, nane, 10?” Alihoji Conte.