Na mwandishi wetu
Wakati fulani mwaka 2000, Yanga ikiwa imetoka kuchukua taji la Ligi Kuu msimu wa 1999/2000 aliyekuwa mwenyekiti wa kamati ya muda ya Yanga, Tarimba Abbas alifanya mkutano na waandishi wa habari.
Baada ya kujibu maswali kadhaa, Tarimba (sasa mbunge Kinondoni) aliwachekesha waandishi alipowaambia kwamba mitaa ya Kariakoo kuna klabu moja ina miaka mingi haijachukua taji.
Tarimba alikuwa akiizungumzia Simba ambayo tangu ichukue taji mwaka 1995 ililisotea hadi kulibeba tena mwaka 2001.
Simba iliyochekwa mwaka 2000, leo hii inashikilia rekodi ya kulibeba taji hilo kwa miaka minne mfululizo yaani 2018, 2019, 2020 na 2021 na kama 2022 watalibeba tena itakuwa rekodi ya kipekee yaani miaka mitano mfululizo (mkono).
Na sasa ligi ikiwa inachanja mbuga swali ni je nani wa kuizuia Simba kutwaa taji la tano mfululizo? Timu zote zinaweza kufanya hivyo lakini inayotajwa zaidi ni Yanga.
Pamoja na ukweli kwamba Yanga ndiyo inayotajwa zaidi lakini inahitaji utulivu wa hali ya juu kung’amua viwango vya Simba na Yanga hasa kwa msimu huu unaoendelea.
Mchezo wa Ngao ya Jamii ndio uliotajwa zaidi kuwa mwanzo wa kuwapa Yanga jeuri na imani kwamba wana timu imara ya kuizuia Simba kutwaa taji la tano mfululizo.
Mchezo ule pamoja na ubora wa Yanga lakini ulituachia maswali fikirishi, kwamba kile kiwango cha Simba siku ile ndiyo inaelekea mwisho wa enzi za utawala au Yanga baada ya kupotea misimu minne imejitathmini upya na kuja kivingine safari hii. Si rahisi kupata jibu la haraka kwa wakati huu.
Si suala la ushindi wa Yanga dhidi ya Simba kwani takwimu zinaisaliti Simba kuwa haina maajabu sana katika mechi zake dhidi ya Yanga hata katika misimu hii yote ikikomba mataji manne mfululizo na kutamba kimataifa.
Kwenye mechi tano za mwisho walizokutana (kwa ujumla), wameshinda mechi moja tu ya Kombe la FA, sare moja (Ligi kuu raundi ya kwanza) na kuchezea kichapo mara tatu (Fainali Kombe la Mapinduzi, Ligi Kuu raundi ya pili, Ngao ya Jamii).
Kwa kuzungumzia kiwango cha kwenye mchezo wao wa Ngao ya Jamii, Simba walizidiwa kwa kila takwimu uwanjani, tofauti na mechi nyingine zote walizokutana hivi karibuni.
Katika mechi ile ya Ngao ya Jamii, Simba walimjaribu kwa mashuti matatu tu kipa Djigui Diarra lakini pia Simba hii ya kupata kona tatu tu ndani ya dakika 90, hasa wakiwa wamefungwa?
Simba tuliyoifahamu ingeipiga Yanga msako wa nyoka lakini kulikuwa na utofauti kadri muda ulivyokwenda, ndivyo Yanga ilizidi kuwabana, kiasi cha kucheza rafu nyingi (26) na kadi nyekundu juu, Thadeo Lwanga.
Simba imeyaanza maisha bila ya Luis Miquissone na Clatous Chama, watu muhimu waliotajwa kuifanya Simba ya sasa ionekane ya tofauti kwani zile ‘one-two’ za Chama pale kati hazipo tena badala yake ‘transition’ yake imekuwa ni kucheza mipira mirefu na spidi ya mawinga (ikumbuke mechi ya Mazembe).
Ingawa Sadio Kanoute na Ousmane Sakho ndio waliotajwa kuwarithi Chama na Luis, bado staili ya uchezaji au ubora wao wameonekana ni watu tofauti.
Kama utaizungumzia mechi ya Ngao ya Jamii, Yanga si tu ilishinda taji bali iliishinda Simba kwa kila kitu. Yanga ilikuwa na kiwango bora siku hiyo, kuanzia kipa hadi safu ya ushambuliaji, ilikuwa na muunganiko, mawasiliano mazuri na kwa tahadhari muda wote.
Kwa ligi ilipofikia pamoja na umuhimu wa mechi za Simba na Yanga ikiwamo ile ya Ngao ya Jamii, bado mechi hiyo haitoshi kuwa kigezo pekee cha kuamini kuwa Yanga wana ubavu wa kuzuia taji la tano kwenda Msimbazi.
Badala yake kinachoonekana sasa ni kwamba timu zote zimeonyesha uhai katika ligi zikishika nafasi mbili za juu, Yanga ikiongoza na pointi 19 ikifuatiwa na Simba yenye pointi 17, kila moja imefungwa magoli mawili, hazijapoteza mechi hata moja, kinachowatofautisha ni matokeo ya sare, Yanga ina sare moja Simba mbili. Matokeo hayo yanatoa picha ya ushindani mkali baina ya timu hizo mbili.
Zaidi ya yote Jumamosi, Desemba 11 timu hizi zitakutana katika mechi nyingine ngumu ya ligi ambayo hapana shaka matokeo yake yatakuwa ni sehemu tu ya furaha au huzuni lakini hayawezi kutoa jibu la moja kwa moja kwamba Simba itatwaa taji la tano mfululizo au Yanga itaizuia Simba kutwa taji la tano.