Na mwandishi wetu
Kocha Mkuu wa timu ya Marumo Gallants ya Afrika Kusini, Dylan Kerr (pichani) amesema anakuja Tanzania kupambana na Yanga akifahamu ubora wa mashabiki wa timu hiyo ikiwa ni miongoni mwa silaha za timu za Tanzania.
Marumo wanatarajia kuvaana na Yanga kwenye mechi ya mkondo wa kwanza ya nusu fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika itakayopigwa Mei 10, mwaka huu kwenye Uwanja wa Mkapa, Dar es Salaam.
Kerr aliyewahi kuinoa Simba msimu wa 2015-16 amesema si mechi rahisi kwao kulingana na ratiba ngumu waliyonayo hivi karibuni hasa kwenye Ligi Kuu Afrika Kusini wanakopambana wasishuke daraja lakini wataipigania ndoto yao ya kutinga nusu fainali Kombe la Shirikisho.
“Binafsi niseme nimeguswa na kuja kwangu tena Tanzania kutokana na ushirika wangu na Simba nilipokuja kuifundisha wakati huo na ni muda mzuri pia kurejea Tanzania kwa sasa.
“Tutakuja kupambana, kufanya kile tulichokifanya kwenye mechi tisa tulizocheza ndani ya siku 28, ni ratiba ngumu tuliyoipitia hasa kwenye ligi lakini nilipofika hapa (Marumo) mara ya kwanza tulionesha kupambana na mpaka hapa tulipofika wachezaji wamefanya kazi kubwa, naamini tutaendelea kupambana,” alisema Kerr.
Kocha huyo raia wa Uingereza alisema anafahamu upinzani wa mashabiki uwanjani atakaokutana nao kutokana na ubora wa ushangiliaji wa mashabiki wa timu za Tanzania akifafanua wamekuwa na utofauti na wa timu nyingine Afrika.
“Niseme mashabiki wa Afrika wamekuwa tofauti kila kanda, Kaskazini wana aina yao kali ya ushangiliaji, sitaki kuwakosea heshima wengine lakini mashabiki wa Simba na Yanga wamekuwa na ushangiliaji ambao umekuwa mzuri na wa kuvutia mno dhidi ya wapinzani,” alisema Kerr ambaye pia amewahi kuinoa Gor Mahia ya Kenya.
Kerr pia aliongeza kuwa timu za Tanzania zinaelekea kwenye mafanikio makubwa Afrika kutokana na uwekezaji uliopo kwenye sekta hiyo akilinganisha na wakati ambao anaiona Simba, akikiri kwa sasa hali ni tofauti.
Marumo inatarajia kurudiana na Yanga Mei 17, mwaka huu kwenye Uwanja wa Royal Bafokeng, Rustenburg, mchezo unaotarajia kupigwa kuanzia saa 1.00 usiku.
