Amsterdam, Uholanzi
Kocha wa Feyenoord ya Uholanzi, Arne Slot (pichani) amesema wazi kuwa ana matumaini ya kuchukua nafasi ya Jurgen Klopp na kuwa kocha mpya wa Liverpool mara baada ya msimu huu.
Liverpool juzi Jumatano ilitangaza kufanya mazungumzo na klabu ya Feyenoord yaliyokuwa na nia ya kumshawishi Slot akabidhiwe majukumu ya kuinoa Liverpool.
Slot kwa upande wake alithibitisha kuwapo mpango huo jana Alhamisi kabla ya timu yake kuumana na Go Ahead Eagles katika mechi ya Ligi Kuu Uholanzi maarufu Eredivisie na kutoka na ushindi wa mabao 3-1.
“Ni kama vile jambo liko wazi kwangu kwamba ningependa kufanya kazi pale, ninachoweza kusema kuhusu hilo ni kwamba klabu kwa sasa zipo kwenye mazungumzo, mimi naendelea kusubiri,” alisema Slot.
Slot aliongeza kuwa anaamini klabu za Liverpool na Feyenoord zitafikia makubaliano na kocha huyo aliyeipa Feyenoord taji la Eredivisie msimu wa 2022-23 ili aanze kazi mpya ya kuinoa Liverpool.
Ili kumpata Slot ambaye pia amewahi kuwindwa na klabu za Tottenham na Leeds, Liverpool italazimika kujadiliana kuhusu ada kwa kuwa katika mkataba wa kocha huyo na Feyenoord hakuna kipengele cha kumruhusu kuondoka baada ya msimu huu.
Jumatano iliyopita nahodha wa Liverpool, Virgil van Dijk ambaye pia ni Mholanzi alisema kwamba falsafa ya soka la Slot itafaa Liverpool na kumtaja kuwa ni kati ya makocha bora kutoka Uholanzi kwa wakati huu.
Slot alianza kuinoa Feyenoord mwaka 2021 na aliwahi kuzungumzia shauku yake ya kuwa kocha katika Ligi Kuu England mwaka jana wakati akihusishwa na mipango ya kujiunga na Tottenham.
Liverpool imemgeukia Slot baada ya kocha wa sasa Klopp, kutangaza Januari mwaka huu kwamba anaachana na timu hiyo baada ya msimu huu, awali Xabi Alonso wa Bayer Leverkusen alitakiwa na timu hiyo lakini akakataa.
