Na mwandishi wetu
Uongozi wa Simba umeeleza kuwa unafahamu timu yao haichezi katika ubora wake lakini wanaamini hilo ni suala la muda na kocha Roberto Oliveira ‘Robertinho’ ataliweka sawa muda si mrefu na Wanasimba watafurahi.
Hayo yameelezwa na Meneja Habari na Mawasiliano Simba, Ahmed Ally baada ya uwepo wa manung’uniko kwa mashabiki wa timu hiyo wakihitaji kuona kiwango cha kuvutia katika mechi zao ingawa timu inapata ushindi.
“Ni kweli bado hatujafikia kile kilele cha ubora wetu kama Simba lakini zipo sababu nyingi za msingi, mojawapo ikiwa ni ugeni wa wachezaji wengi, wachezaji 11 wote wapya na si rahisi kwa idadi hiyo kwa muda mfupi wakazoea na kucheza vizuri kama timu.
“Lakini tunalipongeza benchi la ufundi chini ya kocha Robertinho na wasaidizi wake na wachezaji kwa kazi kubwa, ni muda mfupi lakini wamepambana kuipigania Simba na sasa tuna pointi na mabao sita,” alisema Ally.
Meneja huyo alifafanua kuwa kinachohitajika sasa kwa timu hiyo ili kuendeleza ushindi ni umoja baina ya mashabiki, benchi la ufundi, wachezaji, viongozi akiamini hakuna kinachoshindikana kwenye Nguvu Moja kama ilivyo kauli yao mbiu.
Simba ambao ni mabingwa wa Ngao ya Jamii msimu huu, imeshinda mechi zake mbili za awali za Ligi Kuu NBC, ikiifumua Mtibwa Sugar mabao 4-2 kabla ya kuichapa Dodoma Jiji mabao 2-0 na kukaa kileleni mwa msimamo wa ligi hiyo.