Berlin, Ujerumani
Mwanariadha wa Kenya, Eliud Kipchoge Jumapili hii aliibuka mshindi wa mbio za Berlin Marathon akitumia saa mbili, dakika moja na sekunde nane, akiwa amevunja rekodi aliyoiweka miaka minne iliyopita katika mashindano hayo alipoibuka mshindi akitumia saa mbili, dakika 1 na sekunde 38.
Kipchoge ambaye kwa sasa ana miaka 37, awali aliivunja rekodi ya mwaka 2014 iliyowekwa na Mkenya mwenzake, Dennis Kimento ambaye alitumia muda wa saa mbili, dakika mbili na sekunde 57.
Mwanariadha huyo ambaye ameshinda mashindano ya Marathon mara 15 kati ya 17 alizoshiriki, alionyesha dalili za kufanya vizuri mapema kwani akiwa nusu ya kumaliza mbio hizo tayari alishatumia dakika 59 na sekunde 51 na ikaanza kudhaniwa kwamba angeweza kuwa mwanariadha wa kwanza kuweka rekodi ya kutumia saa mbili tu katika mbio hizo.
Kipchoge aliwahi kushiriki mbio za Marathon za Vienna mwaka 2019 na kuweka rekodi ya kumaliza mbio hizo kwa kutumia muda chini ya saa mbili lakini mashindano hayo hayakuwa yenye hadhi na yanayotambuliwa rasmi.
Mwanariadha wa Ethiopia, Andamlak Belihu, awali ndiye aliyeonyesha kuwa mshindani wa Kipchoge katika hatua za mwanzo mwanzo lakini baadaye alianza kupoteza kasi na kuzidiwa na Kipchoge pamoja na Mkenya mwingine, Mark Korir ambaye alishika nafasi ya pili akitumia 2:04.49 wakati wa tatu alikuwa mwanariadha Tadu Abate wa Ethiopia.
Kwa Kipchoge huo unakuwa ushindi wa nne kwenye Berlin Marathon na hivyo anakuwa ameifikia rekodi iliyokuwa ikishikiliwa na mwanariadha maarufu wa Ethiopia, Haile Gebrselassie.
Akizungumzia ushindi wake, Kipchoge alisema, “Nafurahia maandalizi yangu, na nafikiri nilikuwa nakimbia kwa kasi kwa sababu ya ushirikianao, kila kitu kimetokana na ushirikiano niliopewa.”
Kipchoge pia aliishukuru familia yake kwa namna ambavyo imempa hamasa katika riadha, “kitu kilichonipa hamasa ni familia yangu na nataka kuwahamasisha vijana katika hili, michezo inaunganisha watu na hilo ndilo linalonia hamasa zaidi.”
Kwa upande wa wanawake, mwanariadha wa Ethiopia, Tigist Assefa aliibuka kinara ambaye alitumia muda wa 2:15.37.
Mkenya avunja rekodi yake Berlin Marathon
Green SportsAuthor / Greensports Media LTD
Greensports author
Read also
