London, England
Mshambuliaji wa Man City, Erling Haaland huenda akaikosa mechi ya nusu fainali ya Kombe la FA dhidi ya Chelsea itakayopigwa leo Jumamosi kwenye Uwanja wa Wembley.
Jumatano iliyopita katika mechi ya robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya dhidi ya Real Madrid ambayo Man City ilipoteza na kutolewa kwa mikwaju ya penalti, mshambuliaji huyo hakucheza dakika zote tisini.
Baada ya mechi hiyo, kocha wa Man City, Pep Guardiola alisema kwamba mshambuliaji huyo mwenye umri wa miaka 23 aliomba kutolewa ingawa kocha huyo alisema wataangalia hali itakavyokuwa kabla ya kuamua kama atacheza au la.
“Mechi ilikuwa ngumu, ilijaa upambanaji na yenye kasi kwa pande zote, kuna hali Erling aliihisi kwenye misuli na ndio maana aliniambia hawezi kuendelea na mchezo,” alisema Pep.
Pep alisema kwamba madaktari wa timu hiyo walimwambia kuwa tatizo lilikuwa dogo lakini mpango wao ni kuendelea kuangalia hali yake itakavyokuwa.
Naye kiungo wa timu hiyo, Kevin de Bruyne ambaye pia aliomba kutolewa katika mechi dhidi ya Real Madrid ingawa yeye inadaiwa kwa sasa yuko fiti kuivaa Chelsea.
Man City ambayo msimu uliopita ilibeba mataji matatu ‘treble’ ya Ligi Kuu England (EPL) Ligi ya Mabingwa Ulaya na Kombe la FA, tayari imepoteza taji la Ligi ya Mabingwa Ulaya na sasa imebakiwa na mataji mawili ya kuyatetea ya FA na EPL.