Madrid, Hispania
Mshambuliaji wa Real Madrid, Vinicius Junior amesema kwamba njia pekee ya kupambana na dhihaka za ubaguzi wa rangi kwenye viwanja vya michezo ni kuwaadhibu wanaojihusisha na vitendo hivyo.
Vinicius ametoa kauli hiyo baada ya mchezaji mpira wa kikapu, Yago Dos Santos ambaye anatokea Brazil kama ilivyo kwa Vinicius kujikuta akisakamwa kwa kauli za kibaguzi juzi Jumanne.
“Tuanze kwanza kuwaadhibu hao watu au tuangalie ilivyokuwa hapo kabla,” alisema Vinicius kupitia mtandao wa Twitter kuhusu kuongezeka kwa matukio hayo hivi karibuni.
“Lakini kwa sababu tu hakuna tunachofanya, tutaendelea kupambana sisi wenyewe,” alisema Vinicius baada ya tukio la Dos Santos kudhihakiwa kwa kauli za kibaguzi.
Kuhusu tukio la Dos Santos picha za video vimemuonyesha shabiki mmoja mwanamke akimtamkia kwa sauti ya juu mchezaji huyo akitaja jina la nyani.
Klabu ya kikapu ya Joventut ya HIspania imesema kwamba ipo tayari kushirikiana na mamlaka wakati Shirikisho la Mpira wa Kikapu Brazil (CBB) limelaani tukio hilo na kutaka wahusika waadhibiwe.
“Jinai imerekodiwa kwenye video na ushahidi ni wa haraka na rahisi, CBB tuna imani mamlaka za nchini Hispania zitachukua hatua kwa nguvu ya sheria ili makosa kama haya yasipite bila adhabu kutolewa,” ilifafanua taarifa ya CBB.