Milan, Italia
Kiungo wa Juventus, Paul Pogba hatokuwa fiti kucheza mechi ya robo fainali ya Coppa Italia dhidi ya Lazio jioni ya leo Alhamisi ingawa mshambuliaji, Dusan Vlahovic anatarajia kuwamo kwenye kikosi cha kwanza.
Wachezaji hao ambao wamekuwa wakisubiriwa kwa muda mrefu hatimaye wameanza kurudi ambapo Jumapili watakuwa kwenye benchi katika mechi ya Serie A baada ya kucheza mechi ya kirafiki iliyohusisha kikosi cha akiba.
Vlahovic hakuiwakilisha Juventus katika mechi yoyote tangu Oktoba mwaka jana lakini katika mechi ya kirafiki majuzi dhidi ya Monza aliingia uwanjani dakika ya 65 kuchukua nafasi ya Mattia De Seiglio.
Katika mechi hiyo ambayo Juventus ililala kwa mabao 2-0, Pogba naye alikuwa kwenye benchi lakini kocha Massimiliano Allegri hakumpa nafasi ya kucheza.
“Ukiacha Bonucci (Lonardo) ambaye bado hajawa fiti kabisa, mchezaji mwingine pekee ambaye hatokuwapo kutokana na kutokuwa sawa ni Pogba,” alisema Allegri katika mkutano na waandishi wa habari jana Jumatano.
“Ni bahati mbaya kwamba unapokuwa nje ya uwanja kwa muda mrefu na kuanza kwa kasi kucheza kuna hali ya kujiona kama una maumivu, labda katika wiki chache atakuwa vizuri na katika kiwanngo cha juu,” aliema Allegri.
Pogba hakuwahi kucheza katika mechi yoyote ya ligi ya Juventu tangu asajiliwe kwa mara nyingine na klabu hiyo mwaka jana majira ya kiangazi.
Juventus inakabiliwa na hali ngumu kwenye Serie A ikiwa imenyang’anywa pointi 15 baada ya kubainika kutoa taarifa za uwongo za matumizi ya fedha na sasa imeangukia nafasi ya 10 hivyo ina kazi ya kufanya ili kurudi nafasi za juu.
“Klabu inajua pa kujitetea katika hilo lakini hilo kwetu haliwezi kuwa sababu, ni lazima twende tukafanye kinachohitajika kufanywa,” alisema Allegri.
“Labda ni mara ya kwanza kwa klabu kunyang’anywa pointi 15, tulikuwa nafasi ya tatu na ghafla tumeshushwa chini, sasa tunatakiwa kuanza tena, ni lazima tukabiliane na hali halisi kwa kadri inavyowezekana,” alisema Allegri.