Barcelona, Hispania
Umoja wa Ligi Kuu Hispania ‘LaLiga’ umewasilisha kortini mashtaka kuhusu matukio ya ubaguzi wa rangi dhdii ya mshambuliaji wa Real Madrid, Vinicius Junior katika mechi ya Real Madrid na Barcelona au El Clasico.
Hii inakuwa mara ya nane kwa La Liga kufikisha kortini matukio ya aina hiyo dhidi ya Vinicius ambaye mwaka jana alinukuliwa akilalamikia wanaomfanyia dhihaka za kibaguzi kutochukuliwa hatua zozote.
“Kwa kuzingatia kilichotokea katika mechi ya Barcelona na Real Madrid, matukio ya kibaguzi yasiyovumilika kwa mara nyingine yalishuhudiwa dhidi ya Vinicius, La Liga tumeripoti matukio hayo katika Mahakama ya Barcelona,” ilieleza taarifa ya La Liga.
Katika mechi hiyo iliyochezwa mwishoni mwa wiki iliyopita, Barcelona ilitoka na ushindi wa mabao 2-1 huku Vinicius akiendelea kukumbana na dhihaka za kibaguzi.
Vinicius ambaye pia ni mshambuliaji wa timu ya Taifa ya Brazil amekuwa akikutana na kadhia za aina hiyo mara kwa mara huku mabosi La Liga nao wakifikisha kadhia hizo mahakamani ikiwamo katika mechi za hivi karibuni za Real Madrid dhidi ya Real Mallorca na Real Betis.
Mapema wiki hii klabu ya Mallorca ilisimamisha kadi ya uanachama kwa miaka mitatu kwa mmoja wa wanachama wake aliyebainika kumtolea Vinicius pamoja na mchezaji wa Villarreal Samu Chukwueze maneno ya dhihaka za kibaguzi.
Mwezi uliopita klabu ya Real Valladolid ilisimamisha tiketi za msimu kwa mmoja wa wanachama wake aliyebainika kumtolea Vinicius kauli za dhihaka za kibaguzi katika moja ya mechi za La Liga.
Polisi jijini Madrid kwa sasa wanachunguza tukio la jezi ya Vinicius yenye namba 20 kuvalishwa sanamu na kuwekwa katika daraja moja karibu na uwanja wa mazoezi wa klabu hiyo.
Desemba mwaka jana kupitia mtandao wa Twitter Vinicius aliandika, “Ubaguzi wa rangi unaendelea katika viwanja vya soka na unashuhudiwa kwenye klabu kubwa tena kwa karibu na La Liga hawafanyi lolote. Nitaendelea kuwa imara na kushangilia ushindi wangu na ule wa Madrid.”
Kimataifa Waliomdhalilisha Vinicius kortini
Waliomdhalilisha Vinicius kortini
Read also