
Barcelona, Hispania
Winga wa zamani wa Man United, Adnan Januzaj inadaiwa kwamba anawindwa na klabu ya Barcelona ambayo kocha wake mpya Xavi anahaha kuijenga upya.
Hivi karibuni timu hiyo ilitolewa katika Ligi ya Mabingwa Ulaya na kuangukia kwenye Europa Ligi jambo lililomkera Xavi aliyedai kuwa ingawa watapambana kutwaa taji la Europa lakini hadhi ya Barca ni Ligi ya Mabingwa Ulaya.
Januzaj aliibukia katika akademi ya Man United lakini baada ya kupandishwa kikosi cha kwanza alipata tabu kuwa na namba chini ya makocha Louis Van Gaal na Jose Mourinho.
Baada ya United alizichezea kwa mkopo klabu za Sunderland na Borussia Dortmund hadi mwaka 2017 alipojiunga na Real Sociedad.
Januzaj mwenye umri wa miaka 26 mkataba wake na Sociedad unafikia ukomo mwishoni mwa msimu huu na ingawa ana mpango wa kuongeza mkataba lakini itakuwa vigumu kwake kukataa ushawishi wa kujiunga na Barca licha ya ukweli kwamba klabu hiyo haiko vizuri kifedha.
Kutokana na ukata wa Barca, klabu hiyo imepanga ama imsajili baada ya mkataba wake kuisha au kufanya hivyo Januari mwakani kwa ada ambayo haitowaumiza.
Pamoja na ukata katika klabu hiyo lakini Xavi amedhamiria kuhakikisha kwamba anaimarisha safu ya ushambuliaji wa timu hiyo huku akizingatia hali halisi ya kifedha na awali ilidaiwa kuwa klabu hiyo inamtaka Raheem Sterling wa Man City.
