Na mwandishi wetu
Uongozi wa Yanga umeeleza kuwa umemaliza majadiliano na mchezaji Feisal Salum ‘Fei Toto’ ndiyo maana sasa umeamua kuacha sheria ifuate mkondo wake kwa kumpeleka Shirikisho la Soka Tanzania (TFF).
Yanga imemburuza mchezaji huyo TFF kupitia Kamati ya Sheria na Hadhi za Wachezaji kutafuta hatima ya Fei kuvunja mkataba na timu hiyo licha ya mkataba wake kuonesha unafikia tamati Mei, 2024.
Mjumbe wa Kamati ya Utendaji Yanga, Alexander Ngai amesema kuwa walipofikia wameona hakuna haja ya majadiliano ndiyo maana wameamua kufuata taratibu za soka zinavyotaka.
“Kwa hapa tulipofika naona kama vile milango ya mazungumzo imeshafungwa, tunamzungumziaje zaidi mchezaji ambaye ana mkataba mpaka 2024, ni kama mfanyakazi amekiuka sheria hivyo mpira nao una taratibu, kanuni zake hivyo ni jambo la kufuata sheria zilivyo,” alisema Ngai.
Alisema kuwa wanashangazwa kuhojiwa kama kesi ikiisha wako tayari kumpokea Fei, akifafanua hata wao hawajui wanampokea kutoka wapi wakati ni mchezaji mwenye mkataba anayepaswa kuuheshimu.
Pia ameongeza kwamba Yanga ni taasisi kubwa ndiyo maana inapata matokeo ikiwa na wachezaji wengine licha ya kutokuwepo kwa Fei ambaye amemtafsiri kama msaliti kwa kueleza kuvunja mkataba zikiwa zimebaki siku chache kabla ya mechi yao na Azam FC.
“Kwa usahihi tuwaambie mashabiki na wapenzi wa Yanga kuwa mjadala wa Fei umefungwa, tuache sheria ichukue nafasi yake, hatuna nafasi ya kumuongelea mchezaji mmoja sababu Yanga ni klabu na taasisi kubwa ina wachezaji wengi wazuri.
“Kama mnavyoona inapata matokeo ikiwa na mchezaji yeyote sababu kila mchezaji asiyepata nafasi, akipewa anafanya kazi ya maana. Fei alishaonesha usaliti maana tunajiandaa na mechi ngumu ya Azam yeye analeta taharuki kama alivyofanya wakati tunajiandaa kucheza na Mtibwa (Sugar),” alisema Ngai.
Awali, ilielezwa kuwa pande hizo mbili zinajadiliana kulimaliza hilo kimaongezi lakini imeripotiwa hali imekuwa ngumu kufikia muafaka ndiyo maana Yanga imeamua kutinga TFF.
Vuguvugu hilo liliibuka wiki mbili zilizopita, Fei akiwaaga Wanayanga kuwa amemalizana nao kimkataba kulingana na vipengele vilivyopo kwenye mkataba huo huku Yanga ikidai ni mchezaji wao halali.
Soka Yanga yamaliza mjadala wa Fei Toto
Yanga yamaliza mjadala wa Fei Toto
Green SportsAuthor / Greensports Media LTD
Greensports author
Read also
