Na mwandishi wetu
Aliyekuwa kocha mkuu wa Tanzania Prisons, Fred Minziro amesema amekubaliana na uamuzi wa kumuondoa katika kikosi hicho ingawa amekiri kuondolewa kwenye kipindi ambacho si sahihi.
Minziro ameieleza hayo GreenSports baada ya leo Jumanne uongozi wa Tanzania Prisons kuweka wazi kusitisha mkataba wa mwaka mmoja walioingia na kocha huyo mwanzoni mwa msimu huu kwa manufaa makubwa ya timu hiyo.
“Nimepewa barua jana ya kusitisha mkataba wetu na sasa naelekea nyumbani Dar es Salaam lakini kuna vitu kama maslahi yangu ya kuvunja mkataba bado sijamalizana nao kwa hiyo tutakapimalizana kwenye stahiki zangu hapo ndio tutakuwa tumekamilisha taratibu za kuachana kabisa.
“Ila pia kabla ya kunipa barua ya kusitisha mkataba, nilikutana na uongozi kuwaeleza juu ya maendeleo ya timu kwa ujumla na niliwaeleza kwamba kuna mchakato wa mabadiliko unakamilika muda si mrefu maana timu inaonekana inavyobadilika lakini ndio hivyo nafikiri wameamua wanachoona sahihi,” alisema Minziro.
Kocha huyo ambaye msimu uliopita alikuwa akiinoa Geita Gold amesema kwa sasa hahitaji kuzungumza mengi zaidi anahitaji kupumzika na kuangalia anamalizana vipi kimaslahi na uongozi wa timu hiyo inayoshika nafasi ya 14 ikiwa na pointi 7 baada ya mechi tisa.
Msimu huu Prisons inakuwa timu ya saba kuachana na kocha wake baada ya Simba, Namungo, Mtibwa Sugar, Ihefu, Singida Fountain Gate na Coastal Union kabla hata ya kukamilika kwa mzunguko wa kwanza wa ligi.