Na mwandishi wetu
Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Amos Makalla amewataka waliovamia eneo la uwanja wa klabu ya Simba au Mo Arena, Bunju, Dar es Salaam kuondoka eneo hilo ndani ya siku 60 ili kupisha ujenzi.
Hayo yalisemwa na Makalla alipotembelea eneo hilo leo akiwa na baadhi ya viongozi wa Simba akiwemo Mtendaji Mkuu, Barbara Gonzalez ili kuzindua rasmi ujenzi wa uzio utakaouzunguka uwanja huo.
Akiwatangazia wananchi hao, Makalla alisema kwamba mgogoro uliopo hapo ni mdogo hivyo hataki kuona mkandarasi anakwama katika ujenzi huo kisa wao kwani atabadili tamko na watahama eneo hilo kwa siku 14 tu.
“Tunamaliza mgogoro huu kama tulivyofanya huko nyuma, uzuri wa hapa ni rahisi tu, Simba, Barbara anzeni kazi leo (jana) kwa kuweka uzio, uzio upigwe, mkandarasi aendelee na kazi, nyie mliopo humo ndani tunawapa siku 60 muhame, mjipange muondoke.
“Nisingependa kusikia kwamba kuna wananchi halafu kwa jina la wavamizi wanazuia watu kuendelea na kazi, nikisikia hizo siku 60 zitakuwa nyingi mtaondoka ndani ya siku 14, tumetumia busara tu,” alisema Makalla.
Aidha, Makalla pia alitoa pongezi kwa timu hiyo kwa kuishi katika msemo wa klabu kubwa nchini kwa kuanza mchakato wa kumiliki uwanja wake binafsi, akisisitiza kuwa Simba na Yanga ndiyo timu kubwa na zinapaswa kuonyesha mfano kama wanaouonyesha Simba sasa.
“Kwa hiyo nyinyi (Simba) mmeonyesha ule ukomavu kuonyesha ni klabu kubwa, uwanja huu ukikamilika sio faida kwa Simba tu, ni faida kwa wananchi wote kwa kuchochea biashara maeneno yote ya karibu yatabadilika hata katika hadhi kutokana na uwanja mkubwa wa kisasa,” alihitimisha Makalla.
Naye mwakilishi wa mkandarasi wa Kampuni ya Mega Woodcraft, Jonathan Kibona waliopewa tenda hiyo alieleza kuwa kwa namna walivyojipanga na vifaa madhubuti walivyonavyo kazi hiyo wataifanya kwa spidi kubwa na wanatarajia ndani ya miezi miwili na nusu watakuwa wamemaliza ujenzi wa uzio.
“Zoezi lilichelewa sababu kulikuwa na uvamizi lakini baada ya maelekezo ya mkuu wa mkoa na vifaa vipo tayari ndani ya miezi miwili na nusu uzio madhubuti utakuwa tayari, ukuta utakuwa mkubwa maana ni uwanja mkubwa sana na tayari tumeweka ofisi na vifaa vyote tayari kwa ujenzi,” alisema Kibona.
Naye Barbara alifafanua kwa uchache kuhusu ujenzi huo: “Mwezi uliopita tulisaini mkataba wa ujenzi wa ukuta, kulikuwa na mchakato wa Nani Zaidi na wanachama wa Simba, wapenzi na wadau walichangia zaidi ya Shilingi milioni 150 na zile fedha tukasema kitu cha kwanza tutatimiza wajibu wetu wa kujenga ukuta, kwa hiyo tutaanza na ukuta wakati tunaboresha michoro na kuweka sawa mambo mengine.”
Soka Waliovamia Mo Arena wapewa siku 60
Waliovamia Mo Arena wapewa siku 60
Related posts
Read also