Manchester, England
Kocha wa Man Utd, Erik ten Hag amewalaumu baadhi ya wachezaji wake wakiongozwa na Cristiano Ronaldo ambao walitoka uwanjani Jumapili iliyopita kabla ya mechi yao ya kirafiki dhidi ya Rayo Vallecano kumalizika.
Man Utd katika mechi hiyo iliyopigwa kwenye dimba la Old Trafford ilitoka sare ya bao 1-1 ambapo Ronaldo alicheza kwa dakika 45 za kwanza na kutolewa lakini zikiwa zimesalia dakika 10 mpira kumalizika alionekana na baadhi ya wachezaji wakitoka nje ya uwanja jambo ambalo Ten Hag amesema kwamba halikubaliki.
Ronaldo amekosa ziara ya maandalizi ya msimu wa 2022/23 katika nchi za Australia na Thailand na kwa mara ya kwanza alionekana katika mechi hiyo ya Jumapili lakini hakuweza kuisaidia timu yake kupata ushindi kabla ya kuondoka akiwaacha wachezaji wenzake wakiumana.
“Sisi ni timu, ni wamoja hiyo maana yake ni kwamba unatakiwa ubaki uwanjani hadi mwisho, kwa yeyote aliyehusika kuondoka mapema hili halikubaliki,” alisema Ten Hag.
Ronaldo ambaye kwa sasa ana umri wa miaka 37 mara kwa mara amekuwa akisisitiza azma yake kutaka kuachana na timu hiyo ambayo aliwahi kuichezea miaka ya nyuma kabla ya kutimkia Real Madrid na Juventus, bado ana mwaka mmoja katika mkataba wake lakini shauku ya kutaka kucheza Ligi ya Mabingwa ndiyo inayomfanya atake kuihama timu hiyo ambayo itacheza Europa Ligi.
Man Utd itauanza msimu mpya wa 2022/23 wa Ligi Kuu England Jumapili hii dhidi ya Brighton huo ukiwa mtihani wa kwanza kwa Ten Hag huku baadhi ya wachambuzi wakisubiri kwa hamu kuona kama Ronaldo atapewa nafasi katika mechi hiyo baada ya kukosekana kwenye maandalizi ya timu hiyo kwa kinachoaminika kuwa ni mgomo wa kushinikiza kuondoka.
Kimataifa Ten Hag: Alichofanya Ronaldo hakikubaliki
Ten Hag: Alichofanya Ronaldo hakikubaliki
Read also
