Doha, Qatar
Brazil ikiwa na staa wake Neymar hatimaye imefuzu robo fainali ya Kombe la Dunia kwa kishindo baada ya kuichezesha samba Korea Kusini na kuichapa mabao 4-1 na sasa inasubiri kuikabili Croatia iliyoibwaga Japan.
Neymar ambaye alicheza mechi ya kwanza ya hatua ya makundi dhidi ya Serbia na kuumia kabla ya kukosa mechi mbili zilizofuata dhidi ya Switzerland na Cameroon hatimaye amerudi na ndiye aliyefunga bao la pili la timu hiyo kwa mkwaju wa penalti katika dakika ya 13 baada ya Richarlison kuchezewa rafu, hilo likiwa bao lake la 76 na timu yake ya taifa.
Brazil, moja ya timu zinazopewa nafasi kubwa kulibeba taji la Dunia, ikitandaza soka safi na la uhakika ilikitumia vizuri kipindi cha kwanza kupata matokeo hayo muhimu ambapo kabla ya Neymar, Vinicius Junior ndiye aliyefungua ukurasa wa mabao dakika ya saba akiitumia pasi ya Neymar.
Mabao mengine ya timu hiyo yalifungwa na Richarlison dakika ya 29 kwa pasi ya Thiago Silva wakati bao la nne lilifungwa na Lucas Pagueta dakika ya 36 akiitumia pasi ya Vinícius Júnior.
Baada ya hapo Brazil iliendelela kudhidhirisha umahiri na ubora wake katika soka kwa kuwachezesha Korea Kusini samba lakini nao hawakukata tamaa na mara kadhaa kipa wa Brazil alilazimika kufanya jitihada za kuokoa hatari kabla ya timu hiyo kupata bao pekee dakika ya 76 mfungaji akiwa Paik Seung-ho kwa shuti la umbali wa mita 30.
Brazil sasa itaingia uwanjani kuikabili Croatia ikiwa na uhakika wa kumtumia Neymar ambaye tayari amedhihirisha kuwa fiti ingawa baadaye kocha Tite alimtoa akiwa tayari ametoa mchango mkubwa pengine kwa lengo la kumuepusha na majanga kabla ya mechi ya robo fainali.
Tite aliwahi kulalamika kwamba mchezaji huyo amekuwa akichezewa rafu mara nyingi na kutaka tabia hiyo iachwe.
Croatia ambayo imeitoa Japan kwa mikwaju ya penalti baada ya sare ya bao 1-1, ni wazi itakuwa na kibarua kigumu kwa Brazil inayoonekana kuwa moto.
Kimataifa Brazil yaichezesha samba Korea Kusini
Brazil yaichezesha samba Korea Kusini
Green SportsAuthor / Greensports Media LTD
Greensports author
Read also
