Na mwandishi wetu
Kikosi cha timu ya Simba kimewasili salama leo nchini Morocco tayari kwa mechi yao ya kukamilisha hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Raja Casablanca.
Simba iliyoondoka na wachezaji 13 jana ikitokea Kilimanjaro walikolazimika kulala kwa usiku mmoja baada ya ndege yao kupata hitilafu, ilifika Morocco saa tatu asubuhi sawa na saa sita mchana kwa saa za Afrika Mashariki.
Kabla ya kutua Morocco, Wekundu hao walipokuwa Qatar waliungana na wachezaji wengine wanne waliokuwa Taifa Stars; Aishi Manula, Beno Kakolanya, Mzamiru Yassin na Shomari Kapombe ambao nao walianza safari hiyo wakiwa Dar es Salaam juzi.
Ofisa Habari wa Simba, Ahmed Ally amezungumza na GreenSports kutoka Casablanca na kueleza kuwa mchezaji mwingine aliyeongezeka baada ya kuwasili Morocco ni Pape Sakho aliyekuwa na timu ya taifa ya Senegal.
Alieleza kuwa timu hiyo ilitarajia kufanya mazoezi jana saa nne usiku huu kwenye Uwanja wa Mohamed V, utakapopigwa mchezo huo saa 7 usiku wa kuamkia Jumamosi.
“Kila kitu kipo sawa, tumefika salama hapa Casablanca na leo tutafanya mazoezi kwenye Uwanja wa Mohamed V kwa ajili ya mechi hiyo. Sakho tayari naye ameshafika na sasa tunawasubiri Chama (Clatous), Inonga (Henock) na Saido (Ntibazonkiza) ambao wataingia muda wowote,” alisema Ally.
Alisema kuwasili kwa wachezaji hao kutakuwa kumekamilisha kikosi kamili kuelekea mechi hiyo ambayo Simba inahitaji ushindi kulinda heshima lakini tayari imeshafuzu hatua ya robo fainali.
Katika Kundi C, Raja ipo kileleni kwa pointi 13 ikifuatiwa na Simba yenye pointi tisa, kisha Horoya AC ya Guinea yenye pointi nne na Vipers ya Uganda yenye pointi mbili ambao tayari wameshapewa mkono wa kwaheri katika mashindano hayo.