London, England
Baada ya kipigo cha mabao 2-1 mbele ya Southampton, kocha wa Chelsea, Thomas Tuchel amesema kwamba wachezaji wake wanatakiwa kukaza na kuonyesha mabadiliko ya kifikra.
Kocha huyo Mjerumani amekilalamikia kile alichokiita kuwa ni mabeki kuwa laini laini katika kukaba na hivyo kuwa sababu ya timu hiyo kujikuta ikipoteza mechi ya pili tangu kuanza kwa Ligi Kuu England msimu huu. Awali Chelsea ilifungwa na Leeds mabao 3-0.
Katika mechi hiyo, Chelsea waliokuwa ugenini ndio waliokuwa wa kwanza kupata bao lililofungwa na mshambuliaji mpya wa timu hiyo, Raheem Sterling lakini mabao ya Romeo Lavia na Adam Armstrong yalitosha kuifanya Southampton kutoka uwanjani vifua mbele kwenye uwanja wa nyumbani.
‘Haitoshi kucheza dakika 20 hadi 25 kwa kiwango tunachokitaka, imekuwa rahisi kututoa kwenye uimara wetu, kutufunga, kutuvuga, imekuwa ni rahisi mno, ilitokea hivyo dhidi ya Leeds, tunatakiwa tujue ni kwa nini na lazima tutafute suluhisho,” alisema Tuchel akizungumzia jinsi timu yake ikiwa ugenini ilivyolala mbele ya Leeds.
“Tulipoteza umakini, tulipotea katika mpango wetu, tulikosa ustahimilivu, ikawa rahisi mno kutufunga, wakati wowote unaweza kupoteza mechi na hili sina tatizo nalo lakini katika mechi ambayo unaongoza huhitaji kukubali kupoteza, kukosa majibu katika kipindi cha pili ni jambo linalosikitisha,” alisema.
Tuchel pia alilalamikia janga la majeruhi baada ya kumkosa beki wake Reece James ambaye ni mgonjwa, pia hakuwa na N’Golo Kante wakati Mateo Kovacic aliingia kipindi cha pili kuchukua nafasi ya Ruben Loftus-Cheek aliyeumia.
“Kwa hakika mimi huwa sipendi kufungwa, na hii ni mara ya pili tunashindwa msimu huu na sidhani kama kunakuwa na kazi ngumu kutufunga sisi, na hili ni jambo nisilolipenda,” alisema kocha huyo Mjerumani na kuongeza kuwa haelewi ni kwanini wanajikuta katika mazingira ya kuwa na majeruhi wote wachezaji wa kiungo.
Kimataifa Kocha Chelsea alaumu wachezaji
Kocha Chelsea alaumu wachezaji
Green SportsAuthor / Greensports Media LTD
Greensports author
Read also
