Na mwandishi wetu
Straika anayetajwa kuwaniwa na Yanga SC, Sudi Abdallah (pichani) ingawa amegoma kueleza alikofikia na Yanga lakini ameisifu timu hiyo kuwa hakuna mchezaji asiyetaka kuitumikia kwa sasa.
Sudi raia wa Burundi aliyekuwa akiitumikia Kuching City ya Malaysia amekuwa akitajwa kuwa kwenye rada za Yanga kuja kuziba nafasi ya Fiston Mayele aliyeondoka Jangwani hivi karibuni.
Akizungumza leo Jumanne alipokuwa akihojiwa na kituo cha redio cha nchini humo, Sudi alisema hawezi kueleza chochote kama amewasiliana na Yanga au la kwa kuwa hilo si suala lake lakini akakiri ni timu ya kuvutia.
“Unajua Yanga ni timu kubwa na kila mchezaji anayetaka kufika mbali amekuwa akifiria hilo, japo zipo timu nyingine kubwa kushinda Yanga lakini unaweza kupita Yanga kutokana na vitu vingi.
“Kwanza kulingana na kiwango walichonacho katika ligi, hata kwenye michuano ya Afrika wamekuwa wakifanya vitu vikubwa kabla ya kutolewa na Waarabu (USM Alger katika fainali) kwa hiyo kila mchezaji anaweza kuvutiwa kuwa hapo,” alisema Abdallah.
Mshambuliaji huyo anayeelezwa kuwa yuko huru kwa sasa amewahi kukipiga Al-Naft ya Iraq, Al-Faisaly ya Saudi Arabia, AS Kigali ya Rwanda na Vital’O ya kwao Burundi.
Yanga imeripotiwa kuingia sokoni kutafuta mshambuliaji mpya baada ya kuondoka kwa nyota wao, Mayele anayetajwa kutimkia Pyramids ya Misri huku pia jina la mshambuliaji kinda Muivorycoast, Sankara Karamoko anayekipiga Asec Mimosas likitajwa katika timu hiyo.
Soka Straika wa Burundi aipamba Yanga
Straika wa Burundi aipamba Yanga
Read also