Na mwandishi wetu
Kocha Mkuu wa Mashujaa, Abdallah Mohamed ‘Baresi’ amesema ameandaa dozi nzito kwa kila timu itakayokanyaga Uwanja wa Lake Tanganyika, Kigoma wakiwemo vigogo Simba na Yanga.
Mashujaa ambayo inashiriki Ligi Kuu NBC kwa mara ya kwanza msimu huu kwa sasa inashika nafasi ya tatu kwenye msimamo wa ligi hiyo ikikusanya pointi nne katika mechi mbili ilizocheza kwenye uwanja huo.
Kocha huyo alieleza kuwa lengo lao kuu msimu huu wa kwanza ni kuhakikisha hawapotezi mchezo wa nyumbani lakini pia wanamaliza msimu wakiwa nafasi za juu kwenye msimamo wa ligi.
“Suala la kufukuzia ubingwa niseme kweli siwezi kuliwazia sababu huu ndio msimu wa kwanza kushiriki ligi kuu, bado tunahitaji uzoefu kwa misimu miwili hivi baada ya hapo tutaanza kufikiria ubingwa lakini katika kipindi chote hicho mkakati wetu ni kuugeuza uwanja wa nyumbani kuwa shubiri kwa mgeni bila kujali ni timu gani tunacheza nayo,” alisema Baresi.
Kocha huyo alisema yeye na wasaidizi wake wamejipanga kuhakikisha wanajenga kikosi imara kitakachotoa upinzani na kupata matokeo mazuri, siyo tu kwenye uwanja wa nyumbani bali hata mechi watakazocheza ugenini.
Baresi pia alisema anafurahishwa na hamasa kubwa kutoka kwa mashabiki wa mkoa huo ambao wamekuwa wakitoa sapoti kubwa kwa timu hiyo pindi inapocheza nyumbani na amewaomba waendelee kuwa hivyo hata watakapocheza na timu za Simba na Yanga.
Mashujaa ilianza vyema ligi msimu wa 2023-24 kwa kuifunga timu kongwe ya Kagera Sugar mabao 2-0 kisha ikatoka sare ya bao 1-1 na Geita Gold, mechi zote zikichezwa Uwanja wa Lake Tanganyika.
