Na mwandishi wetu
Straika wa zamani wa Yanga, Yusuph Athuman (pichani) na Eric Mwijage aliyekuwa Kagera Sugar wametemwa rasmi na timu waliyokuwa wakiitumikia ya West Armenia inayoshiriki Ligi Kuu ya Armenia.
Wachezaji hao ambao kila mmoja alikuwa na mkataba wa miaka miwili, Julai mwaka huu walipewa rasmi mkono wa kwaheri baada ya kumalizika kwa mikataba hayo na timu hiyo.
Taarifa iliyopatikana kupitia mtandao wa West Armenia, ilieleza kuhusu uamuazi wa klabu hiyo kuwaacha wachezaji watano ambao mbali na Watanzania hao, wengine ni Andre Mensalao, Westherley Garcia na Eydison Soares.
“Mikataba na wachezaji wafuatao wa soka ilikatizwa kwa makubaliano ya pande zote mbili: Andre Mensalao, Aidison Soares, Westerly Garcia, Eric Edson Mwijage, Yusuph Athuman. Kwa niaba ya klabu, tunawashukuru kwa kazi waliyofanya,” ilieleza taarifa hiyo.
Timu ya West Armenia imemaliza ligi nchini humo ikiwa nafasi ya nane kati ya timu 10 baada ya kukusanya jumla ya pointi 17, ikishinda mechi tano, sare mbili na kupoteza 13.
