Saudi Arabia
Saudi Arabia imeteuliwa kuwa mwenyeji wa fainali za Fifa za Kombe la Dunia la Klabu ikiwa ni nchi ya sita kupewa uenyeji tangu kuanzishwa kwa michuano hiyo mwaka 2000.
Nchi hiyo imetangazwa kuwa mwenyeji ikiwa ni siku chache baada ya Real Madrid kubeba taji hilo jijini Rabat, Morocco baada ya kuilaza Al-Hilal ya Saudi Arabia kwa mabao 5-3.
Waziri wa Saudi Arabia anayehusika na masuala ya michezo alisema kwamba nafasi yao kuwa mwenyeji wa michuano hiyo itakayofanyika Desemba mwaka huu inaashiria nchi yao kuelekea kuwa tishio kwenye soka.
Saudi Arabia katika miaka ya karibuni imekuwa ikiwekeza kwa kiasi kikubwa kwenye michezo licha ya kutuhumiwa kwa mambo kadha wa kadha ya kijamii ikiwamo ukiukwaji wa haki za binadamu.
Nje ya hilo, inadaiwa tayari nchi hiyo imeanza kuziogopesha baadhi ya nchi zinazowania uenyeji wa fainali za Kombe la Dunia kwa namna ambavyo imekuwa ikiimarisha miundombinu ya soka.
Ni hivi karibuni tu Fifa imejikuta ikilaumiwa baada ya habari kuibuka kwamba shirikisho hilo lina mpango wa kuifanya mamlaka ya utalii Saudi Arabia kuwa mdhamini wa fainali za Kombe la Dunia kwa wanawake za 2023.
Saudi Arabia tayari imepata uenyeji wa fainali za Kombe la Asia mwaka 2027 lakini pia nchi hiyo inawania kuwa mwenyeji wa fainali za Kombe la Asia kwa wanawake mwaka 2026 na hapo hapo inawania kuwa mwenyeji wa fainali za Kombe la Dunia.
Kimataifa Saudi Arabia mwenyeji Kombe la Klabu
Saudi Arabia mwenyeji Kombe la Klabu
Read also