Na mwandishi wetu
Kocha Mkuu wa Polisi Tanzania, Mwinyi Zahera (pichani) amesema timu hiyo haishuki daraja na matumaini yao ya kuepuka kushuka daraja yanaanza Ijumaa hii kwa kuifunga Singida Big Stars.
Polisi Tanzania itaikabili Singida kwenye Uwanja wa Liti, Singida ukiwa ni mchezo wa raundi ya 26 wa Ligi Kuu NBC.
Zahera ameendelea kusisitiza kuwa timu yake haitoshuka daraja msimu huu licha ya kushika nafasi ya mwisho kwenye msimamo wa ligi hiyo inayoelekea ukingoni.
“Tumefanya maandalizi ya kutosha kipindi hiki ambacho ligi ilisimama kwa muda, tulicheza mechi tatu za kirafiki ambazo naamini zimetuimarisha na kurekebisha makosa yetu ndio maana hata mchezo wa keshokutwa dhidi ya Singida Big Stars naamini tunashinda,” alisema Zahera.
Kocha huyo ameeleza kuwa anajua watu wengi hawaamini maneno yake lakini mechi tano zilizobaki zinatosha kabisa kuiweka timu yake sehemu salama.
Alisema amekuwa akizungumza na wachezaji wake na kuwaeleza umuhimu wa mechi zilizobaki anaamini kila kitu kitakwenda vizuri na watu watakubaliana na yeye baada ya ligi kumalizika.
Polisi Tanzania ina pointi 19 katika michezo 25 iliyocheza hadi sasa na ili kuepuka kushuka daraja inalazimika kushinda michezo yote huku ikiziombea mabaya timu za Ruvu Shooting, Prisons na Coastal Union.
