Manchester, England
Kocha wa Man United, Ruben Amorim amesema itakuwa ni jambo la ajabu kufikiria kwamba ataruhusiwa kuendelea kuinoa timu hiyo kama wataendelea kupata matokeo mabaya.
Kwa hali ilivyo nafasi ya Amorim ipo njia panda, haina tofauti na mtu aliyekalia kuti kavu wakati huu timu hiyo ikiwa nyumbani Old Trafford kuumana na Sunderland, leo Jumamosi Oktoba 4, 2025 katika mechi ya Ligi Kuu England (EPL).
Amorim, kocha kutoka nchini Ureno hadi sasa ameshinda mechi tisa tu kati ya 33 za EPL tangu akabidhiwe jukumu la kuinoa timu hiyo takriban miezi 10 iliyopita, rekodi ambayo si nzuri na mechi ya leo dhidi ya Sunderland inaweza kumpa matumaini ya kuendelea na timu hiyo au kufifisha matumaini hayo.
Akifafanua zaidi kuhusu mazingira yanayomkabili, Amorim amesema kuwa ni jambo lisilowezekana kwa mmoja wa wamiliki wa klabu hiyo, Sir Jim Ratcliffe kuendelea kuwa na imani naye kama kiwango cha uchezaji cha timu hiyo hakitabadilika.
“Hakuna hapa mtu ambaye si mzoefu, tunaelewa kwamba tunahitaji matokeo mazuri kuendelea kuwa hapa, tunaweza kufika mahala ambapo hali itakuwa isiyowezekana kwa kila mtu kwa sababu hii ni klabu kubwa yenye wadhamini wengi na wamiliki wawili,” alisema Amorim.
Kati ya mechi tisa alizoshinda Amorim, nne zilipatikana dhidi ya timu ambazo zilipanda EPL ambazo ni Ipswich, Burnley, Southampton na Leicester.
Kwa Sunderland hata hivyo hali inadhaniwa kuwa tofuati kwani ni kama imeshazowea mikiki ya EPL ikiwa tayari imekusanya pointi 11 katika mechi sita za awali mwanzo ambao si mbaya kwa timu ambayo ndiyo kwanza inapambana EPL ikitokea Championship.
Amorim amekuwa akikabiliwa na hoja za mara kwa mara kumtaka abadili mfumo anaoutumia kwa timu yake wa 3-4-3 lakini mara zote amekuwa akisisitiza kwamba hatobadili mfumo huo.
Akitetea mfumo huo Amorim alisema kwamba yeye ni kocha wa klabu kubwa lakini anashangaa ni vyombo vya habari vinavyompangia nini akifanye jambo ambalo amesema haiwezekanni kulivumilia.
