Na mwandishi wetu
Timu ya soka ya Wanawake ya Simba Queens leo Jumapili inashuka dimbani kuwakabili mabingwa wa Wanawake Morocco, AS FAR katika mchezo wa ufunguzi wa Ligi ya Mabingwa Afrika utakaochezwa nchini Morocco.
Awali kabla ya mchezo huo wa Simba unaotarajia kupigwa majira saa 2.00 usiku Uwanja wa Moulaye Hassan, kwanza utatanguliwa na mchezo wa kwanza baina ya Green Buffaloes ya Zambia dhidi ya Dertermines Girls ya Liberia. Hiyo yote ikiwa ni michezo ya Kundi A.
Hii ni mara ya kwanza Tanzania na Afrika Mashariki kwa maana ya ukanda wa Cecafa inawakilishwa na timu ya wanawake kutoka nchini baada ya msimu uliopita ambao ni wa kwanza wa michuano hiyo kuwakilishwa na Vihiga Queens ya Kenya.
Queens chini ya Kocha Charles Lukula inaamini itafanya vizuri kwenye mashindano hayo baada ya kufanya maandalizi mazuri kwa muda mrefu.
Kinachowapa jeuri hiyo, ni namna walivyosajili kuelekea michuano hiyo huku wakijipima kwa mechi mbalimbali za kirafiki kujiweka imara, mechi ambazo wamedai zimewapa majibu mengi kuelekea mashindano hayo yatakayomalizika Novemba 13, mwaka huu.
Lukula alisema hivi karibuni kuwa amewasoma wapinzani wake kwa muda mrefu na anajua namna ya kukabiliana nao huku akisisitiza kuwa sapoti anayoipata kutoka kwa uongozi wa klabu hiyo anaamini utawafikisha kwenye malengo ya kufanya vizuri hatua ya makundi na kuingia nusu fainali.
Mbali na kundi hilo, kundi B linaundwa na timu za Bayelsa Queens ya Nigeria, Wadi Degla ya Misri, TP Mazembe ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo na mabingwa watetezi Mamelodi Sundowns ya Afrika Kusini.
Kimataifa Simba Queens kibaruani Morocco
Simba Queens kibaruani Morocco
Green SportsAuthor / Greensports Media LTD
Greensports author
Read also
