London, England
Tottenham Hotspur imethibitisha kuwa Ange Postecoglou ndiye kocha mpya wa timu hiyo baada ya kusaini mkataba wa miaka minne na hivyo kuwa kocha wa kwanza kutoka Australia kuinoa timu ya Ligi Kuu England (EPL).
Postecoglou (pichani) mwenye umri wa miaka 57 ambaye hapo kabla alikuwa akiinoa Celtic ya Scotland, ataanza rasmi kazi katika klabu hiyo Julai Mosi huku mwenyekiti wa Spurs, Daniel Levy akiamini kocha huyo atafanya kazi yake vizuri.
“Ange atabadili mtazamo na kwa haraka atakuwa na timu yenye mfumo wa kushambulia, ana rekodi nzuri ya kuwaendeleza wachezaji na mwenye uelewa kuhusu umuhimu wa muunganiko wa kuanzia kwenye akademi,” alisema Levy katika taarifa yake.
“Kila kitu ni muhimu kwa klabu yetu, tumefurahishwa kwa Ange kuungana nasi wakati huu tukijiandaa kwa ajili ya msimu ulio mbele yetu,” aliongeza Levy.
Habari za Alhamisi iliyopita zilidai kwamba Spurs iliwasiliana na mabosi wa Celtic kuhusu kumtaka kocha huyo na mazungumzo yakaenda vizuri jana Jumatatu na kwa haraka baada ya Postecoglou mwenyewe kuonesha shauku ya kutaka kuinoa timu ya EPL.
Postecoglou ambaye ameiwezesha Celtic kubeba mataji matatu ya ndani msimu huu, anarithi mikoba ya kocha Mtaliano Antonio Conte ambaye mambo yalimshinda katika klabu hiyo na kuamua kuondoka.
