Paris, Ufaransa
Kocha wa PSG, Luis Enrique kwa mara nyingine amemtupa benchi mshambuliaji wake tegemeo Kylian Mbappe katika mechi dhidi ya Monaco iliyochezwa jana Ijumaa na kuisha kwa sare ya 0-0.
Enrique ambaye alisema huo ni uamuzi wake na alichukua hatua hiyo wakati wa mapumziko hii ikiwa ni mara ya pili baada ya kuchukua hatua kama hiyo wiki iliyopita katika mechi dhidi ya Rennes ambayo pia iliisha kwa sare.
PSG kwa sasa ndiyo inayoshika usukani wa Ligi Kuu Ufaransa au Ligi 1 kwa tofauti ya pointi 12 na Enrique amerudia kauli yake ya awali kwamba ni lazima wajiandae kuishi bila ya Mbappe ambaye anahusishwa na mipango ya kuhamia Real Madrid.
“Nimekuwa kwenye soka kwa muda mrefu kiasi cha kutosha, lazima mfahamu kwamba kila kitu ni muhimu katika klabu ya aina hii, hivi karibuni au hapo baadaye tutacheza bila ya Mbappe, kwa hiyo naangalia mbadala muhimu kwa ajili ya timu,” alisema Enrique.
“Kuna wakati nakuwa sahihi na kuna wakati nanya makosa, tunahitaji kuzowea kucheza bila ya Mbappe, nitakuwa nafanya kila kilicho bora kwa timu yangu, sihitaji kuibua utata, huu ni uamuzi wangu,” alisisitiza Enrique.
Enrique pia alisema kwamba hakuwa akifahamu kwamba Mbappe aliangalia mechi hiyo kipindi cha pili akiwa jukwaani pamoja na mama yake badala ya kwenye benchi la timu hiyo ingawa baada ya mechi aliungana na wachezaji wenzake uwanjani.