Na mwandishi wetu
Mchezaji wa timu ya Taifa ya Wanawake, ‘Twiga Stars’ Aisha Masaka amewahimiza wasichana wenzake kupambana zaidi kwani kuna fursa za kutosha kucheza ligi za nje ya nchi.
Masaka ambaye alipata umaarufu kupitia Yanga Princess ameeleza kuwa ipo nafasi kwa wasichana wengi kucheza soka la kulipwa Ulaya kinachohitajika kwao ni kujituma sehemu walipo ili kujiuza.
“Naamini wasichana wenzangu wadogo na wenye ndoto ambao wanatamani kufika huku niliko inawezekana, ni kujitahidi kuonesha kipaji chako watu wakikuona siku moja na wewe pengine ukauzwa kunako klabu nyingine kubwa za Ulaya,” alisema.
Masaka anayekipiga BK Hacken ya Sweden amekuwa akionesha kiwango bora katika timu hiyo, akiisaidia kufanya vizuri kwenye michuano ya Ligi ya Mabingwa Ulaya ya Wanawake.
Hacken ipo Kundi D ya ligi hiyo ikiongoza kwa pointi sita ikifuatiwa na Chelsea yenye pointi nne, Real Madrid inayomiliki pointi moja na PSG inayoburuza mkia bila ya pointi.
Mbali na Masaka, Watanzania wengine wanaocheza soka la kulipwa ni Opa Clement aliyewahi kuitumikia Simba Queens kwa sasa anacheza Beskitas ya Uturuki, Enekia Kasongo anayecheza Eastern Flames na Clara Luvanga anayecheza Al Nasri zote za Saudi Arabia.